Na,Enock Magali,Dodoma
Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Dodoma kimesikitishwa na ufaulu hafifu unaosababisha mkoa kushika nafasi za mwisho kitaifa huku kikimtaka Afisa Elimu wa mkoa wa Dodoma ajitafakari na akiona ameshindwa kupandisha ufaulu aachie ngazi.
Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa CCM wa mkoa huo Godwin Mkanwa wakati akichangia hali ya elimu katika mkoa wa Dodoma katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya mkoa huo kilichofanyika jijini hapa.
“Muungwana ni vitendo ,ukiona uungwana umekushinda jiengue mwenyewe,kwa hiyo Afisa Elimu jipime ,kama mambo yameshindikana ,chakula hakiivi ,nyanyua mikono,
“Kasome ilani ya CCM ,kama huwezi kuitekeleza pisha,tunataka mabadiliko ya kifikra na kiutendaji.”alisema Mkanwa
Aliongeza kuwa,yeye kama kiongozi aliyekabidhiwa dhamana ya Elimu anatakiwa kuonyesha njia ya nini kifanyike ili mkoa uweze kuongeza ufaulu na kuondoka katika nafasi za mwishoni kitaifa hususani katika matokeo ya darasa la saba.
Akichangia hoja Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kongwa White Zuber alisema aliwahimiza wajumbe wa kikao hicho kuimarisha vikao vya wadau katika kila wilaya kuzungumzia masuala ya elimu na kutatua changamoto za kielimu zinazowakabili.
Alisema,suala la chakula cha mchana linapaswa kupewa kipaumbele hata kwa shule za mijini kwa lengo la kuwafanya watoto kuvutiwa kukaa shuleni kusoma.
”Suala la chakula liwe la mkoa mzima,watoto wale chakula ,sisi Kongwa tumeanza na ufaulu unaendelea vizuri ,jamii lazima ichangie .”alisema Zuber
Naye Mbunge wa Mtera Livingstone Lusinde alisema ,mimba bado ni tatizo kwa watoto wa kike huku akisema mwaka huu pekee wanafunzi tisa wamepata katika shule ya Mvumi Misheni.
Awali akiwasilisha taarifa ya maendeleo yua elimu mkoani humo,Afisa Elimu huyo alisema katika matokeo ya darasa la saba mwaka 2018 mkoa wa Dodoma umeshuka nafasi mbili na kushika nafasi ya 19 kutoka nafasi ya 17 mwaka 2017,hali iliyoamsha ari ya wajumbe.

No comments:
Post a Comment