We are currently working on a new website.
Stay tuned for more information.

to stay updated on our progress.

Thursday, February 28, 2019

Mrisho Mpoto amtolea maneno mazito Diamond 'Ruge amefariki njoo umzike'



Baada ya kuenea kwa taarifa za msiba wa Mkurugenzi wa vipindi na uzalishaji, Clouds Media, Msanii wa nyimbo za asili Mrisho Mpoto amemtaka Msanii wa Muziki ambaye tangu Mkurugenzi huyo afariki hajaposti chochote hivyo amemuomba msanii huyo kwenda kumzika.

Mrisho Mpoto  amemuomba msanii huyo aende akamzike Ruge, kama anamheshimu na kumsikiliza.

"Nasib Abdul nimekwita jina lako la kuzaliwa mimi kama kaka yako unaeniheshimu na kunisikiliza nakwambia. RUGE MUTAHABA AMEFARIKI nakuomba NJOO UMZIKE... Nimemaliza," ameandika Mrisho Mpoto kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Tangu kutokea kwa msiba huo hata Media yake ya Wasafi Tv hawajaandika chochote kuhusiana na msiba huo ila wasanii walio chini ya lebo yake ya WCB wamendika kuhusu msiba huo kupitia kurasa zao za Instagram.


Serikali Yatoa Ajira Mpya 4,549 kwa Walimu na Maelekezo Yake

Imewekwa Tar.: February 28th, 2019
Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania imetoa fursa ya ajira zaidi ya elfu nne kwa Walimu wa Shule za Msingi na Sekondari  ili kupunguza changamoto ya uhaba wa walimu mashuleni nchini.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(OR-TAMISEMI) Mhe.Selemani Jafo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika  ukumbi wa Reform uliopo katika ofisi za OR - TAMISEMI Jijini Dodoma.
Mhe. Jafo amesema kuwa sasa ni wakati wa walimu wenye sifa kuchangamkia fursa ya ajira kwa kutuma maombi yao kwa njia ya mtandao kupitia kiunganishi mtandao cha http://ajira.tamisemi.go.tz (Online Teacher Employment Application System-OTEAS).
“Muombaji awetayari kufanya kazi sehemu yoyote kwani sisi tutapanga kulingana na maeneo yenye uhitaji wa walimu wenye sifa husika katika maeneo hayo kwani sisi ndio tunajua wapi kuna upungufu wa walimu” ameeleza Mhe.Jafo
Mhe.Jafo ametoa  wito kwa waombaji  wote watakaopata nafasi hizo kwenda kufanya kazi kwa moyo mmoja na weledi wa juu ili kuhakikisha watanzania wananufaika na elimu inayotolewa na wao, na hapo changamoto ya uhaba wa walimu katika sekta ya elimu itakuwa imetatuliwa.
Aidha, Mhe. Jafo amesema Walimu wanaotakiwa kutuma maombi ni wenye sifa za kitaaluma, Walimu wa Shule za msingi Daraja la IIIA wenye Astashahada ya Ualimu, Walimu Daraja la IIIB wenye Stashahada (Diploma) ya Ualimu katika masomo ya Kiingereza, Uraia, Historia, Jiografia na Kiswahili.
Walimu wa Daraja la IIIC wenye Shahada ya Ualimu kwa masomo ya Kiingereza,  Uraia,  Maarifa ya Jumla (General Studies), Historia, Jiografia na Kiswahili.
Huku sifa nyingine ya walimu wa shule za msingi ikiwa ni mwalimu wa Daraja la IIIC wenye Mahitaji Maalum aliyehitimu shahada ya ualimu kwa masomo ya Englishi, Civics, General studies, history, Jeiography na Kiswahili.
Huku sifa za walimu wa shule za Sekondari ni walimu wa Daraja  la IIIC wenye shahada  ya ualimu waliosomea elimu maalum, Walimu Daraja la IIIB wenye shahada (Diploma) ya Ualimu waliosomea elimu maalum, walimu wa Daraja IIIB wenye shahada, Daraja la IIIC katika masomo ya Sayansi ya Kilimo, Uchumi wa Nyumbani (Home Economics), Fizikia, Hisabati, Kemia na Biolojia.
Mhe. Jafo ameongezea kuwa sifa za jumla kwa waombaji ni sharti awe mtanzania, awe amehitimu kati ya mwaka 2014 hadi 2017 isipokuwa kundi maalum la wahitimu wa Elimu ya Ualimu wa masomo ya Fizikia na Hisabati hawa hawana muda maalum wa kuhitimu, lakini asiwe na umri wa miaka 45 wakati anatuma maombi na walimu waliowahi kuomba na hawakupata nafasi, wanapaswa kutuma maombi upya.
Amehitimisha kwa kusema barua zote za maombi ziambatishwe na nakala ya vyeti vya taaluma, utaalamu na kuzaliwa ambapo mwisho wa kupokea maombi hayo ni tarehe 15 mwezi Machi, 2019.

Dudu Baya Mikononi mwa Polisi Kisa Ruge


Dudu Baya Mikononi mwa Polisi Kisa Ruge

Msanii wa muziki Bongo, Dudu Baya leo anatarajiwa kufika kituo cha Polisi Posta Dar es
Salaam mara baada ya kupigiwa simu na polisi na kutakiwa kufanya hivyo.
Utakumbuka mapema jana Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt.Harrison
Mwakyembe aliliagiza Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) kwa kushirikiana na Polisi kuhakikisha
wanamkamata Msanii DUDU BAYA kwa kosa la kukashifu na kutoa lugha za kejeli kwa Marehemu
Ruge Mutahaba.
Hatua hiyo ilifikiwa mara baada ya Dudu Baya kutumia ukurasa wake wa mtandao wa Instagram kutoa lugha isiyofaa kimaadili kwa Marehemu Ruge.
Ruge Mutahaba ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji Clouds Media Group (CMG)amefariki siku ya jana nchini Afrika Kusini alipokuwa akipatiwa matibabu ya figo. Ruge alizaliwa mwaka 1970, Brooklyn nchini Marekani, atakumbukwa zaidi kwa mchango wake mkubwa katika sekta ya muziki nchini

🔴 LIVE: TAARIFA YA HABARI YA ITV SAA MBILI USIKU 28 FEBRUARI 2019..


Wasanii walivyoguswa na kifo cha Ruge Mutahaba


TASNIA ya habari na burudani nchini imepata pigo kubwa kwa kuondokewa na Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Kampuni ya Clouds Media Group (GMG), Ruge Mutahaba.
Kiongozi huyo amepoteza maisha nchini Afrika Kusini alikokuwa anapatiwa matibabu. Taarifa za kifo hicho zilianza kusambaa majira ya saa 12 jioni baada ya kifo chake kutokea saa 10:30
Ruge kwa muda mrefu alikuwa anasumbuliwa na maradhi ya figo hadi alipopatwa na umauti.
Alikuwa mmoja kati ya watu walioupigania muziki wa Bongo Fleva hadi kufikia hapo ulipo kwa sasa, hivyo wasanii mbalimbali wameoneshwa jinsi walivyoguswa na msiba huo mzito.
Elias Barnaba
Huyu ni mmoja kati ya wasanii ambao wameguswa na kifo cha mkurugenzi huyo. Kupitia ukurasa wake wa Instagram, aliandika:
“Tazama hapa mzee baba amka, Ruge jamani moyo wangu mbovu jamani baba sitaki, amka Mungu wangu jamani, baba naumia jamani, naumia hapana baba nimekuimbia wimbo jana nikaomba angalau utumiwe usikie baba sasa wee moyo wangu hauna nguvu tena,” aliandika hivyo.
Barnaba ni mmoja kati ya wasanii ambao wamepata umaarufu kupitia kwa Ruge, msanii huyo alikuwa mmoja kati ya zao la Tanzania House of Talent (THT) ambayo ilianzishwa na Ruge.
Mwasiti Almasi
Ukizungumzia mazao ya THT, huwezi kuliacha jina la Mwasiti Almasi, alikuwa mmoja kati ya wasanii waliotangazwa na kituo hicho kwa wasanii wa kwanza kabisa kutambulika na muziki wa Bongo Fleva.
Yeye ni mmoja kati ya wasanii walioshindwa kuzuia hisia zake hasa pale alipokuwa anahojiwa na kujikuta akitokwa na machozi mara zote.
“Mungu wangu hili tabasamu hatulioni tena, uwii dah inaumiza sana, Ruge aliwahi kuniambia, Mwasiti nawapenda sana wadogo zangu mkitimiza ndoto zenu ndio faraja yangu, daa umeenda boss Ruge jamani umeenda boss jamani uwii siamini,” aliandika hivyo kwenye ukurasa wake wa Instagram.
Ambwene Yesaya ‘Ay’
Ni mmoja kati ya wasanii wanaoamini kuwa Ruge alikuwa na mchango mkubwa katika tasnia ya burudani nchini, hivyo kwenye ukurasa wake wa Instagram aliandika: “Pumzika kwa amani kaka yetu Ruge Mutahaba, tutakukumbuka kwa mengi uliyofanya poleni sana Clouds FM, Cloud TV ndugu jamaa na marafiki.”
Mwana FA
Kutokana na kuguswa sana na kifo hicho, Hamis Mwinjuma hakuwa na mengi ya kuandika kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii, aliposti picha ya moyo ukiwa umechanika na kuandika neno Ruge.
Maneno mafupi kama vile Pumzika Pema Peponi Bosi Ruge Mutahaba, yaliandikwa na wasanii mbalimbali ikiwa pamoja na Joseph Haule maarufu kwa jina la Professor Jay. Upande wake msanii Aslay Isihaka aliandika kwa kifupi: “Mungu akupe kauli thabeet father huko uendapo.”
Nikki wa Pili
Rapa kutoka kundi la Weusi, Nickson Simon, ni mmoja kati ya wasanii waliotumia kwa upana sana ukurasa wao wa Instagram kwa kuandika yale ya moyoni baada ya kupata taarifa ya kifo hicho.
“Tunachonga barabara kamata fursa, tunakufungulia dunia, hayo yote yanamaanisha wengi wanakumbuka kwa kuwapa njia.
“Lakini nini maana ya njia? uliamini njia huanza kwa kukata msitu na kupasua milima hivyo endelevu, lazima kuhusisha kijiji hadi mkoa, barabara moja mpaka njia nne, njia isiyoendelea hupitwa na wakati, njia huboa baadhi ya vijiji, njia hupata lawama lakini ndio iletayo maendeleo, njia hubeba walio wema na wabaya, misiba na harusi, njia hupiganiwa ndio maana kuna mistari ili kupunguza ugomvi lakini ajali hutokea.
“Njia si mali yako unaweza pitwa na yeyote ukaporwa kijiti na njia kuu ni lazima utaiacha, kumbuka kutengeneza njia ya kwenda bomani kwako hivyo lazima kupambana, R.I.P Genius,” aliandika Nikki.
Amini
Ni miongoni mwa zao la THT, hivyo msanii huyo alipofanya mazungumzo na mwandishi wa makala haya, alisema kwa kushirikiana na wasanii wenzake waliotokea kwenye kundi hilo, watahakikisha wanaifanya THT iendelee kuishi kama alivyopanga Ruge.
Kala Pina
Amedai ataendelea kumkumbuka Ruge kwa kuwa alimpa wazo la kuanzisha kipindi cha Dawa za Kulevya kupitia Clouds TV.
“Nitaendelea kumkumbuka Ruge kwa kuwa wazo la kipindi ambacho alinipa kiliweza kusaidia kuwabadilisha vijana kwa namna tofauti huku wengine wakiacha kabisa kutumia dawa za kulevya,” alisema Kala Pina.
Alisema wazo la kuanzisha kipindi hicho lilitoka kwa Ruge, atamkumbuka Ruge kupitia kipindi hicho kwa kuwa aliweza kusababisha watu kuacha dawa za kulevya.
Kala Jeremiah
Msanii huyo amedai kwamba, mwaka 2017 aliitwa na Ruge na kumshauri namna ya kufanya muziki wake ili kuweza kuwafikia vizuri mashabiki wake.
Hata hivyo, katika mazungumzo hayo, alimwambia kuna kitu ambacho watakuja kukifanya, lakini kwa bahati mbaya hadi anapoteza maisha juzi hawajaweza kufanya lolote.
Steve Nyerere
Amewataka wasanii na wadau mbalimbali nchini kumsamehe Ruge Mutahaba kama waliwahi kukosewa na mwasisi huyo wa THT.
“Binadamu tujifunze kusamehe, najua wapo watu ambao walikosewa na Ruge, hivyo wanatakiwa kusamehe na wale wote ambao wanatumia mitandao ya kijamii kwa kuandika maneno ya kejeli juu ya Ruge ni vizuri wakachukuliwa hatua, ili ni pigo kubwa kwa wasanii wote hadi wa filamu kwa kuwa alikuwa na mchango sehemu zote,” alisema Steve.
Mr Blue
Yeye aliandika: “Pumzika kwa amani kaka yetu kipenzi, Ruge Mutahaba Mungu kakupenda zaidi.”
Wakati huo huo, Zuwena Mohamed maarufu kwa jina la Shilole, aliandika: “Kwa hiyo sikuoni tena na tabasamu lako jamani Ruge, Mungu akupokee baba yetu umeacha pengo kubwa sana kwa wengi wenye upendo wa kweli na wewe kwenye tasnia tunalia, nani atatusaidia tena saini ya kwenda America na sehemu zingine, kila nafsi itaonja umauti.”
Kwa mujibu wa msemaji wa familia ya Ruge, Anneck Kashasha, mwili wa marehemu utaingia kesho Ijumaa na kuagwa Jumamosi kwenye Ukumbi wa Karimjee na kusafirishwa Jumapili kuelekea Kagera na mazishi yatafanyika Jumatatu.

Picha : LOWASSA AFIKA NYUMBANI KWA RUGE MUTAHABA KUWAFARIJI WAFIWA




Waziri Mkuu Mstaafu na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Edward Lowassa na mkewe Mama Regina Lowassa leo asubuhi wamefika nyumbani kwa Prof. Mutahaba ambaye ni baba mzazi wa Ruge Mutahaba aliyekuwa mkurugenzi wa uzalishaji vipindi wa Clouds Media Group kutoa pole na kuwafariji wafiwa.


Ruge Mutahaba Alifariki dunia Juzi nchini Afrika Kusini alikokuwa akipatiwa matibabu ya figo zilizoanza kumsumbua mwaka jana.


Mwili unatarajiwa kuwasili jijini Dar es salaam kutokea Afrika Kusini siku ya kesho Ijumaa, Machi 1, 2019.







Alikiba na mkewe wapata mtoto



Msanii wa muziki wa Bongo Fleva, Alikiba na mkewe wamefanikiwa kupata mtoto wao wa kwanza siku ya jana, vyanzo vya kuaminika vimeeleza hivyo.

Utakumbuka alfajiri ya April 19, 2018 (alhamisi) Alikiba alifunga ndoa na Mrembo Aminah Rikesh Ahmed huko mjini Mombasa nchini Kenya.

Pia siku hiyo ndio kwa mara ya kwanza Alikiba alitambulisha kinywanji chake cha Mofaya ambacho pia kwa mara ya kwanza kilionekana kwenye wimbo wake uitwao Mvumo wa Radi kwa lengo la kukitangaza (product replacement).

Pia ndani ya mwezi huo (April 22, 2018) mdogo wake na Alikiba, Abdu Kiba naye alifunga ndoa ambapo walifanya sherehe ya harusi pamoja ndani ya Serena Hotel kama nilivyotangulia kueleza.

RAIS DKT. MAGUFULI AKUTANA NA MAKAMU WA RAIS MTENDAJI MWANDAMIZI WA JICA KAZUHIKO KOSHIKAWA IKULU JIJINI DAR ES SALAAM

 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akiwa katika mazungumzo na Makamu wa Rais Mtendaji Mwandamizi wa Shirika la Kimataifa la Ushirikiano la Japan (JICA) Bw. Kazuhiko Koshikawa (wa tatu Kushoto) na ujumbe wake walipokutana Ikulu jijini Dar es salaa leo Februari 28, 2019. Wa pili kulia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt Damas Ndumbaro.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akimpa zawadi ya picha ya kuchora ya wanyama wakuu watano (Big Five) Makamu wa Rais Mtendaji Mwandamizi wa Shirika la Kimataifa la Ushirikiano la Japan (JICA) Bw. Kazuhiko Koshikawa alipokutana na kufanya naye mazungumzo Ikulu jijini Dar es salaa leo Februari 28, 2019. Kulia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt Damas Ndumbaro.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akimpa zawadi ya kinyago ja UJAMAA Makamu wa Rais Mtendaji Mwandamizi wa Shirika la Kimataifa la Ushirikiano la Japan (JICA) Bw. Kazuhiko Koshikawa alipokutana na kufanya naye mazungumzo Ikulu jijini Dar es salaa leo Februari 28, 2019. Kulia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt Damas Ndumbaro.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli katika picha ya pamoja na Makamu wa Rais Mtendaji Mwandamizi wa Shirika la Kimataifa la Ushirikiano la Japan (JICA) Bw. Kazuhiko Koshikawa (wa tatu Kushoto) na ujumbe wake baada ya kukukutana na kufanya naye mazungumzo Ikulu jijini Dar es salaa leo Februari 28, 2019. Wa pili kulia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt Damas Ndumbaro.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akiagana na Makamu wa Rais Mtendaji Mwandamizi wa Shirika la Kimataifa la Ushirikiano la Japan (JICA) Bw. Kazuhiko Koshikawa (wa tatu Kushoto) na ujumbe wake baada ya kukukutana na kufanya naye mazungumzo Ikulu jijini Dar es salaa leo Februari 28, 2019. Wa pili kulia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt Damas Ndumbaro.
PICHA NA IKULU

Ratiba ya awali ya mazishi ya Ruge na mahali atakapozikwa yawekwa wazi (+ Video)



Ikiwa ni siku ya huzuni kwa Watanzania baada ya kuondokewa na mtu muhimu sana katika sekta ya burudani ambaye alikuwa msaaka vijana wengi sana pia akiibua vipaji vya vijana mbalimbali na kuvikuuza, huyu sio mwingine bali ni Mkurugenzi wa vipindi na uzalishaji wa Clouds media Group, Bwana Ruge Mutahaba ambaye mpaka sasa ni marehemu baada ya kupoteza maisha akiwa kwenye matibabu nchini Afrika ya kusini.


Mpaka sasa famili imeshatoa ratibu fupi ya awali ya mazishi ya Ruge:-


Tetesi za Soka Ulaya Alhamisi 28.02.2019: Lukaku, QPR, Wilson, Jovic, Vukovic

Romelu Lukaku ameifungia Manchester United mabao 36 katika mechi 77

 Romelu Lukaku ameifungia Manchester United mabao 36 katika mechi 77

Mshambuliaji wa Ubelgiji Romelu Lukaku, 25, anapania kujiunga na Juventus endapo atalazimishwa kuondoka Manchester United. (Sun)

QPR huenda wakahamia uwanja wao mpya wenye uwezo wa kuhimili mashabiki 45,000 kama sehemu ya mradi wa maendeleo uliyogharimu euro milioni 425. (Mail)

Meneja wa Leicester Brendan Rodgers anataka kutumia euro milioni 40 kumjumuisha mshambuliaji wa Bournemouth na England Callum Wilson, 27 katika kikosi chake. (Sun)


Manchester City wanamfuatilia mshambuliaji wa Benfica na Serbia Luka Jovic, ambaye anaichezea Eintracht Frankfurt kwa mkopo. (Mail)
Chelsea ni miongoni mwa vilabu vya ligi ya Primia vinavyomtafuta kiungo wa kati wa Croatia na Maritimo Josip Vukovic, 26. (Talksport)

Arsenal imemuita nyumbani kipa wake Emiliano Martinez ambaye amekuwa akichezea Reading kwa mkopo.

Emiliano anatarajiwa kuwa mlinda lango wa pili kwasababu hawana uwezo wa kumnunua kipa mwingine kuchukua nafasi ya Petr Cech anayeelekea kustaafu. (Sun)


Meneja wa Leeds United David Hockaday anasema alijaribu kumsajili mlinzi wa sasa wa Liverpool na Uholanzi Virgil van Dijk kutoka Celtic alipokuwa Elland Road, lakini ombi lake lilikatalliwa na mmiliki wa klbu hiyo Massimo Cellino. (Guardian)

Chelsea imewauliza mashabiki wake katika mtandao wa Twitter kupendekeza mchezaji ambaye wanataka asajiliwe na klabu hiyo licha ya marufuku ya usajili wa wachezaji inayowakabili. (Reuters)

Mshambuliaji wa Manchester United James Wilson, 23, anasema kuwa aliamua kuhamia Aberdeen kw amkopo msimu huu ili ''kujiuza''. (ESPN)

Real Madrid inapania kumnunua beki wa kushoto wa Ajax muargentina Nicolas Tagliafico, 26, kuchukua nafasi itakayoachwa wazi na Marcelo. (Tuttosport, via Mirror)

Marcelo ambaye ni nyota wa kimataifa wa Brazil anajiandaa kujiunga na Juventus. (Tuttosport, via AS)

Manchester United inamfuatilia kiungo wa kati wa Barcelona na Croatia Ivan Rakitic, 30. (Mail)

Juventus haina mpango wa kumrudisha tena mshambuliaji wa kimataifa wa Argentina Gonzalo Higuain katika klabu hiyo mkataba wake wa bure utakapokamilika Chelsea. (Il Corriere di Torino, via Sun)

Kipa wa Uhispani David de Gea, 28, anakabiliwa na hatari ya kushuka thamani nje ya Manchester United, licha ya klabu hiyo kuwa tayari kumpatia mkataba mpya wa euro £350,000 kwa wiki. (Evening Standard)

Kipa wa Ajax na Cameroon Andre Onana, 22, yuko katika orodha ya kuwa kipa mpya wa Barcelona endapo Jasper Cillessen, 29, ataondoka klabu hiyo. (El Club de la Mitjanit, via Sport)

Steve Nyerere: Dudubaya Anapaswa Kuomba Msamaha


Steve Nyerere: Dudubaya Anapaswa Kuomba Msamaha


Muigizaji nguli wa filamu nchini, Steve Nyerere, amesema kama kuna msanii anamzungumzia vibaya marehemu Ruge Mutahaba kwa sasa jkama anavyofanya Rapa Dudu Baya basi anapaswa kutengwa kwani hakuna binadamu aliye mkamilifu.
  • Steve amesema Ruge amefungua milango kwa vijana wengi na kutoa fursa waweze kufanikiwa huku akiweka wazi kuwa atamkumbuka milele

Nyota Mwingine mtanzania apata timu ulaya


Ile ndoto ya watanzania wengi kucheza kimataifa huenda ikazidi kufanikiwa kwani leo nyota mwingine kutoka Singida United ameelekea nchini Czech kucheza soka la Kulipwa.
Singida United kupitia ukurasa wao wa twitter wameandika ujumbe Huu hapo chini.
Klabu ya Singida United imefanikiwa kumpelekea mchezaji John Tibar George namba 7 Mgongoni kwenye club ya Mfk Fc iliyopo Jamhuri ya Czech.
Tibar anaondoka saa 5:00 Usiku wa leo akipitia Ufaransa ambako atakaa kwa muda usiopungua wiki moja kwenye club Toulouse Fc kwaajili ya fitness na techniques.
Vibali vyote vimeshatumwa kwenye club yake mpya ikwepo ITC.Hivyo anakwenda huko kuanza maisha ya soka moja kwa moja.
Tunashukuru sana wote waliohusika kufanikisha hili, zaidi TFF kwa ushirikiano wao wote katika kipindi chote cha kuhakikisha vibali vya mchezaji huyu vinapatikana kwa wakati.
Huu ni mwendelezo wa Singida United kuendelea kuwafungulia njia wachezaji wakitanzania kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya Tanzania. Tutaendelea kufanya hivi kwa maslahi ya, klabu, timu ya Taifa na wachezaji wenyewe

Watu 7 Wafikishwa Mahakamani Mauaji ya Watoto Njombe


Watu saba wamefikishwa mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Njombe  kwa tuhuma za mauaji ya watoto mkoani Njombe yanayohusishwa na imani za kishirikina.

Mmoja wa watuhumiwa hao ni David Kasila ambaye alifikishwa kwa mara ya kwanza mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Njombe februari 18 mwaka huu akituhumiwa kuwaua watoto watatu ambao ni Oliver Ng’ahala(5),Goodluck Mfugale(5)Meshack Myonga(4) wote ni wakazi wa wilaya ya Njombe.

Watuhumiwa wengine ni Mariano Malekela,Edwini Malekela,kalistus Costa wakazi kijiji cha Matembwe tarafa ya Lupembe walifikishwa mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Njombe mnamo februari 19 mwaka huu kwa tuhuma za kumuua mtoto wao Rachel Malekela(7) februari moja mwaka huu ambapo mwili wake ulikutwa mita 50 kutoka nyumbani kwao akiwa amechinjwa.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana kamanda wa polisi Mkoa wa Njombe Renata Mzinga,alisema kati ya watuhumiwa 49 waliokuwa wakishikiliwa na jeshi la polisi baada upelelezi watuhumiwa saba pekee ndio walikutwa na hatia na kufikishwa mahakamani kwa tuhuma hizo.

‘’Hata hivyo oparesheni zetu ziliendelea hadi tulipofika mikoa jirani ya Mbeya,Iringa na hata Songea ambako tuliweza kuwapata watu mbalimbali pamoja na msako wetu tuliendelea kuwakamata waganga wa jadi na hasa wale wapiga ramli chonganishi ambao waliweza kuchochea chuki katika mkoa wetu’’alisema Renata.

Alisema jeshi la Polisi  limewafikisha mahakamani watu saba,watatu kwa tukio la mauaji ya watoto watatu kijiji cha Ikando,mtuhumiwa mmoja kwa mauaji ya watoto watatu mjini Njombe,na watuhumiwa watatu kwa mauaji ya mtoto mmoja kijiji cha Matembwe.

Alisema kutokakana na oparesheni iliyofanyika wanaendelea kuwaomba wananchi kuendelea kutoa taarifa za mtu yoyote atakaebainika na kuwa na dalili zozote za kujihusisha kwenye mauaji hayo.

‘’Tunaomba wananchi waendelee kutuletea taarifa ambazo ni za kweli. taarifa ambazo zitaweza kutusaidia sio taarifa za fitina au za kukomoa watu wakidai kuwa wanajihusisha na matukio haya kwa mfano wananchi wanaotuletea taarifa za maandishi wakieleza kuwa kuna matumizi ya gari namba zimehifadhiwa,kuna watu walioshuhudia majina yamehifadhiwa kuna gereji zinazotumika kuficha waalifu jina la gereji limehifadhiwa hapo itatuletea ugumu  sisi polisi kukamilisha upelelezi wetu’’alisema.

‘’Tunaomba taarifa za kueleweka ili kuweza kukomesha mauaji haya moja kwa moja sio taarifa ambazo zinaeleza majina yamehifadhiwa,sisi tunazichukulia kama taarifa za majungu ambazo hazina utafiti wowote na haziwezi kutuletea mafanikio.pia wananchi waendelee kutuletea taarifa za waganga wa jadi hasa wale wapiga ramli chonganishi ili tuwakamate na kuwafikisha mahakamani’’alisema Renata.

Pia Kamanda huyo amewataka wazazi na walimu kuendelea kushirikiana kuwalea watoto sambamba na kuwaasa wananchi waache kuamini imani za kishirikina na badala yake wafanye shughuli halali ili waweze kuhakikisha jamii inakuwa salama.

Kamanda Mzinga alisema wananchi wazingatie taratibu za kisheria kwa ajili ya kutatua migogoro ya ardhi na wafuate taratibu za mirathi ili kuepuka kufanya mgawanyo wa mali kwa kutumia ubabe na visasi.

Aidha jeshi la polisi  mkoa wa Njombe linaendelea na upelelezi juu ya mtoto Gaudes Kihombo(7) mkazi wa kijiji cha Ikando kata ya Kichiwa aliyepotea tangu Januari sita ambaye hadi sasa hajapatikana.

Mpaka sasa watuhumiwa saba wamefikishwa mahakama ya hakimu mkoa wa Njombe kwa matukio ya mauaji ya watoto nane wakiwemo wa familia moja.

Azam FC yawafungia wachezaji wake




Uongozi wa klabu ya Azam FC imesema kuwa kuanzia sasa haitoruhusu wachezaji wake kwenda kufanya majaribio katika klabu zingine na kama itawahitaji basi zinatakiwa kufuata utaratibu maalum.

Hayo yameelezwa na Afisa Habari wa klabu hiyo, Jaffar Iddy Maganga, akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es salaam ambapo amesema kuwa uongozi wa klabu hiyo hautaruhusu mchezaji yeyote wa timu yake hasa kutoka timu za vijana kwenda kufanya majaribio katika timu nyingine.

"Kwanza kabisa wanafahamu kuwa wachezaji wanaotoka hapa ni Superior kwasababu kuna kila kitu. Kwahiyo hatuwezi kupeleka timu ambayo tunajua kabisa uwezo wake ni mdogo, na sisi tunafuatilia lakini tunajua wenyewe jinsi gani tunafuatilia", amesema Jaffar Idd Maganga.

Hatua hiyo imefikiwa ili kuweza kujenga umara wa kikosi chake na kupoteza muda kwa wachezaji hao.

Kikosi cha Azam FC hivi sasa kipo chini ya kocha wa vijana chini ya miaka 20, Meja mstaafu Abdul Mingange na Idd Cheche wa timu ya vijana chini ya miaka 17, baada ya Kocha Mkuu, Hans van der Pluijm kutimuliwa hivi karibuni baada ya mfululizo wa matokeo mabovu

Habari Kubwa Zilizoandikwa Kwenye Magazeti Ya Leo Alhamisi Februari 28.2019














TANGAZO LA NAFASI ZA AJIRA ZA WALIMU WA SHULE ZA MSINGI NA SEKONDARI, FEBRUARI 2019

Bofya hapa kuzitazama..

Video: Ommy Dimpoz akutana na Steve Nyerere ‘Tusahau yaliyopita’



Ni Ommy Dimpoz na Steve Nyerereambao wasanii hao wawili siku kadhaa zilizopita waliwahi kuchukua headlines mitandaoni, sasa leo Feb 27, 2019wamekutana kwenye msiba wa Ruge Mutahaba na wamekubali mvelewamemaliza tofauti zao na kuanza safari mpya.

CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM) CHATOA SALAMU ZA POLE KUFUATIA KIFO CHA MKURUGENZI WA VIPINDI WA CLOUDS MEDIA GROUP, RUGE MUTAHABA




Mambo ya kuzingatia wakati wa kuchagua mpenzi wa kuishi naye


Wakati wa kuchagua mwenzi wako wa kuishi ni lazima uweze kujipanga  katika suala la kufanya maamuzi, hii ni kwa sababu hakuna kazi ngumu hapa duniani kama kuchagua mwenza wa kuishi naye.

Yafutayo  ndiyo mambo ya msingi ya kuzingatia ili kuchagua mwenzi wa kuishi naye:

Chagua mtu mwenye huruma.
Mtu anayeelewa maumivu yako na anayeweza kufanya jitihada za kukuweka sawa pindi unapokuwa katika kipindi kigumu. Chagua mtu mwenye fadhila na mwenye ukarimu; mtu ambaye ana moyo wa huruma, na asiyeogopa kuionesha huruma yake kwa vitendo.

Chagua mtu ambaye haogopi kufunguka.
Amini nakuambia, ni jambo salama sana kuwa na mtu asiye na tabia ya kuyaficha maumivu yake moyoni mwake. Na mojawapo ya hali inayoogopesha zaidi katika mapenzi ni ile hali ya kutoweza kujua anachokiwaza mpenzi wako hasa kuhusu wewe. Watu ambao hawako tayari kueleza kinachowasibu au dukuduku zao hujitengenezea bomu la matatizo bila kujijua, bomu ambalo hata lisipolipuka leo linaweza kulipuka muda wowote siku moja bila hata kujua sababu; unaweza kuwa vizuri sana. Naamini umewahi kusikia mikasa ya watu ambao mapenzi yao yaliisha bila ya wao kutarajia, mume au mke anarejea nyumbani kutoka kazini anakuta mwenza wake amekusanya kilicho chake na kuondoka.

Chagua mtu ambaye anataka kuwa karibu na wewe, kimwili na kihisia.
Chagua mtu anayependa kuwa karibu kihisia na kimwili; mtu ambaye hachoki kuzungushia mkono wake shingoni, begani, kiunoni au kushikilia mkono wako; mtu ambaye anapenda kukubusu. Kugusa kunaweza kuongeza radha yamapenzi katika uhusiano. Na kwa kuchagua mtu ambaye anaonekana kufurahia kuzungumza na wewe. Mtu ambaye hapendi ujisikie mpweke.

Chagua mtu ambaye ana maadili mema na mnayeshabihiana.
Unaweza kupuuzia na kuchukulia kuwa hili ni jambo dogo tena halina maana ya msingi, lakini nakuambia kuwa mtu asiyependezwa na yale unayofurahia anaweza kuishiia kuvuna janga la upweke utakao pelekea kutelekezwa. Na hatimaye wanaweza kumtafuta mtu mwingine ambaye wanaendana naye. Ikiwa wewe ni mkimbiaji, tafuta mkimbiaji; ikiwa wewe ni mwandaaji mziki, tafuta mtu anayevutiwa na muziki; ikiwa wewe ni mtu wa ibada, mtafute mtu anayependa ibada pia!.

Kufuata ushauri wangu sio njia ya uhakika kwamba hamtatengana. Kwa hakika utakuwa na mambo mengine machache ya kuyazingatia kama; kuwa na tabia njema kwa mpenzi wako, kuwa na heshima, na uwe mwepesi wa kutatua matatizo.

Mpaka kufikia hapo sina la ziada nikutakie siku njema.

Wednesday, February 27, 2019

Serikali yasimamisha leseni ya gazeti la The Citizen kwa Wiki Moja


Serikali imesimamisha leseni ya uchapishaji na usambazaji wa gazeti la The Citizen kwa siku 7 kuanzia leo, Februari 27, 2019, kwa madai ya kuandika habari ya uongo na upotoshaji kuhusu kuporomoka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania.

Barua ya Februari 27, 2019 ya kusimamishwa kwa The Citizen iliyosainiwa na msajili wa magazeti, Patrick Kipangula kwa niaba ya Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) inaeleza kuwa adhabu hiyo inahusu pia mtandao wa gazeti hilo.

“Katika habari hiyo kwa makusudi uliandika habari za uongo na upotoshaji kwa kuaminisha umma wa Watanzania na kwamba thamani ya Shilingi ya Tanzania imeporomoka ikilinganishwa na miaka mitatu iliyopita pasipo kufuata utaratibu wa kisheria na kanuni za fedha ambapo viwango vya fedha ya Tanzania hutolewa na Benki Kuu ya Tanzania,” inasema aya mmojawapo ya barua hiyo.

 “Uamuzi wa kusimamisha kwa muda leseni hiyo unatokana na mwenendo na mtindo wa habari na makala ambao kwa kiasi kikubwa unakiuka misingi ya maadili ya taalamu ya habari kwa upotoshaji wa mara kwa mara wa taarifa zinazohusu Serikali na uchochezi bayana unaokiuka masharti ya leseni,” inasema aya nyingine katika hiyo iliyotumwa kwenda kwa Mhariri Mtendaji Mkuu wa Mwananchi Communications Limited (MCL).

Katika barua hiyo, Serikali imeeleza kuwa licha ya gazeti la The Citizen kuomba radhi mara kwa mara bado limeendelea na uandishi ule ule wenye utata na ikalitaka lijirekebishe na kuzingatia misingi ya taalamu ya habari na sheria za nchi.

Mkurugenzi wa Idara ya Habari amesema licha ya habari hiyo, The Citizen limewahi kuchapisha habari nyingine inayokiuka misingi na maadili ya uandishi wa habari Julai 22, 2018.  

Habari hiyo iliyokuwa na kichwa cha habari ‘US Senator Raises Alarm on Tanzania” ilimnukuu seneta wa Jimbo la New Jersey nchini Marekani, Bob Menendez alieleza kuhusu mwelekeo wa ukuaji wa demokrasia nchini Tanzania.

Mh Mwakyembe Aagiza Dudubaya Kukamatwa



Waziri anaeshughulikia maswala ya michezo nchini amefunguka na kutoa amri kukamatwa kwa msanii Dudubaya ambae alianza kutoa maneno ya kashaf kwa marehemu Ruge Mutahaba ambae amefariki siku ya jana jioni,.

Marehemu Ruge alifariki akiwa katika matibabu yake nchi Afrika ya Kusini , huku msanii Dudubaya akiwa ameanza kurusha maneno ya kejeli na matuzi kwa mkurugenzi huyo ambae alikuwa akipigania afya yake tangu akiwa hai.

Hata baada ya kifo, msanii dudubaya aliendelea kutuma maneno ya kejeli katika mitandao ya kijamii na kukwaza watu wengi na hata kuanza kumlili awaziri mwenye dhamana hiyo kutaka kumchukulia hatau msanii huyo.

Hata hivyo baada ya saa chache tangu kuripotiwa kwa msanii huyo , tayari msanii huyo ameamuriwa kukamatwa na kuwekwa ndani ili kuthibiti hali hiyo.

Taarifa hiyo ambayo imetolewa na naibu waziri wa habari ,sanaa na micheoz mh juliana shonza anasema kuwa kwa kushirikiana na BASATA na polisi wanatakiwa kumkamata msanii DUDUBAYA.

Naibu Waziri, Subira Mgalu amkalia kooni Mkandarasi



Naibu waziri wa Nishati, Subira Mgalu ametoa wiki moja kwa mkandarasi wa ujenzi wa miundombinu ya umeme,kampuni ya State Grid  Electrical and Technical Works kumaliza kazi ya kuunganisha umeme katika vijiji vya Mtama baada ya kuchelewa kumaliza kazi hiyo kwa takribani miezi sita.

Mgalu alitoa agizo hilo baada ya baadhi ya wananchi wa kijiji cha Mihogoni kumlalamikia kuhusu kuchelewa  kuunganishwa umeme katika vijiji vyao.

Wananchi hao walisema  kuchelewa kwa mradi wa  umeme katika eneo lao kunasababiswa na uzembe wa mkandarasi anayejenga mradi huo.

Walisema ni vyema serikali ikaangalia uwezekano wa kubadilisha makandarasi ili mradi huo ukamilike kwa wakati

Baada ya kusikia malalamiko na maombi ya wananchi hao, Mgalu alisema serikali haiwezi kuwavumilia watendaji au wakandarasi wanaofanya kazi kwa mazoea. Kwahiyo mkandarasi huyo akamilishe zoezi la kupanda nguzo za umeme na kuwasha ndani ya siku saba alizompa.

Alisema  serikali inatambua umeme ni biashara sio anasa,hivyo  vijiji 30  vilivyopo kwenye mpango katika wilaya Lindi na 133 vya mkoa wote wa Lindi vitapate umeme.

Kwa upande wake, Meneja Mradi wa kampuni ya  State Grid Electrical and Technical Works Mhandisi, Bahati Manyangali alikiri kuwepo kwa ucheleweshaji  wa umalizaji wa kazi hiyo.Hata hivyo alisena uchelewaji huo ulikotokana na sababu za kiufundi na kuchelewa  nguzo za umeme

Alisema tayari kazi ya kupanda nguzo 10  kati ya 30 zinazotakiwa kupandwa katika kijiji cha Mihogoni  imeanza.



Waziri Makamba Aandika Waraka Mzito…..”Ruge, naomba nisikilize kidogo. “

Waziri Makamba Aandika Waraka Mzito....."Ruge, naomba nisikilize kidogo. "

Ndugu yangu Ruge, najua ndio umewasili huko upande wa pili na si ajabu una mambo mengi na bado unasalimiana na jamaa zetu wengi waliotangulia.
Lakini naomba uchukue muda wako kidogo kunisikiliza. Nimeumia sana na nimelia peke yangu kwamba umetuacha namna hii. Sawa, umeitwa kwa wakati wako na sisi hatuna kauli kwenye suala la wakati wa kuitwa lakini nilitegemea, na sikuwa na shaka kabisa, kwamba tutakamilisha yale mawazo yako mengi mazuri uliyoniambia. Sikuwa na shaka kwasababu nilishuhudia pale Hospitali ya Kairuki kabla hujaenda India, ulivyorudi kutoka India, na siku nimekuona Afrika Kusini, ulivyokuwa unapigana kupona — hadi madaktari wa Afrika Kusini wakakupa jina “Ruge, The Fighter”. Jina sahihi kabisa lililotafsiri harakati za maisha yako.
Unajua nini? Nilikuwa nangoja urudi Dar nikwambie nilichogundua mara ya mwisho nilivyokuona hospitali. Lakini ngoja tu nikwambie kabla sijaja huko uliko. Ile kiu kubwa ya kupona niliyoiona kwenye macho yako haikuwa kwa ajili yako wewe, bali kwa ajili ya kutoiangusha familia yako nzima iliyosimamisha kila kitu kukuuguza na Watanzania wote waliokuwa wanakuombea. Ulipigana kupona, sio kwa ajili yako, bali kwa ajili yetu. Hukuamka kitandani lakini hukushindwa mapambano kwasababu umeamkia ndani ya mioyo ya Watanzania. Huku tuliko karibu watu wote tunakumbuka ulivyotugusa. Jamaa yangu, tunakuomboleza wakati huu, halafu tutabaki tunafurahia nuru yako katika maisha ya wengi kwa urefu wa uhai wetu. Umekimbia mbio njema, umemaliza safari yako vyema.
Majonzi yangu ni kwamba umeondoka kabla sijalipa kwa ukamilifu deni langu kwako. Deni la upendo na urafiki wa kweli. Ulinipa heshima kubwa ya kuwa msiri wako — kwa kuniamini na kunielezea wasiwasi wako, ndoto zako, matumaini yako, harakati zako, mipango yako. Ulinipa heshima ya kunipa fursa ya kubishana nawe kuhusu mawazo na fikra zako.
Majonzi yangu ni kwamba kuna vitu fulani vikubwa na vizuri tulivipanga — mimi na marafiki na wadogo zako, kwa ajili yako, kwa staili yako — mapema mwezi Machi, ambavyo naamini vingekupa tabasamu. Kama unaweza, hapo ulipolala, tupe ishara tufanyeje.
Nafarijika kidogo kwamba nilipata nafasi ya kukukumbatia kwa mara ya mwisho. Sikujua kwamba tunaagana. Ulinishika mkono kwa nguvu, hukutaka kuuachia, na ulitabasamu niliposema nakungoja Dar tukae pale THT, kama kawaida yetu, kujadili mawazo na mipango yako mingi.
Ingawa umeshawasili huko upande wa pili, familia yako na watu wengi watauaga mwili wako kwa heshima kubwa. Utajengewa kaburi. Nadhani litawekwa marumaru. Lakini tukitaka kukusalimia tena hatutakutafuta kaburini kwako. Tutakutafuta kwenye nyoyo za watu uliowagusa na kuwasaidia. Na ni wengi kweli. Kumbukumbu yako itabaki kwenye nyoyo zao na kwenye mafanikio yao. Watoto wako hawapo peke yao. Watalia sana, lakini ni kwa muda tu; kwasababu watafunikwa kwa upendo wetu sote na watafarijika, na watakuwa na fahari, kwa jinsi unavyosemwa na unavyokumbukwa.
Ndugu yangu, nisikuchoshe. Mengine tutaongea tutakapokutana tena kwasababu kwa hakika sisi sote, mmoja mmoja na kwa wakati wetu, kwa kadri ya mipango ya yeye aliyetuumba, tutakufuata huko. Miaka yote nimekujua, sijawahi kukuona umepumzika. Pumzika kwa amani kwa sasa — na milele.
Ndimi, rafiki yako,
January Makamba
27 Februari 2019

Tuesday, February 26, 2019

NAFASI ZA AJIRA ZILIZO TANGAZWA LEO JUMANNE


Systems Administrator Job at HR World limited











Msimamo wa CUF Upande wa Maalim Seif baada ya Prof. Lipumba kuteua bodi mpya

Leo February 26 2019 Wabunge wa CUF upande wa Maalim Seif wameiomba mahakama kuharakisha maamuzi ya kesi na kuamua uhalali wa Mwenyekiti wa Chama hicho Profesa Lipumba, kwani kuchelewa kufanya maamuzi kunapeleka kuendelea kwa mgogoro kwenye chama hicho hali inayoathiri utendaji kazi wa wabunge.

Watumishi Wa Umma Nchini Marufuku Kutumika Kisiasa

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) amewataka watumishi wa umma nchini kutotumika kisiasa kwani uwepo wao una lengo mahususi la kuboresha utoaji huduma wenye viwango stahiki ikiwa ni pamoja na kuijenga Serikali ili iweze kuleta maendeleo kwa wananchi.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri huyo wakati wa kikao kazi na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao, kabla ya kutembelea wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wilayani Kisarawe ili  kujiridhisha na utekelezaji wa mpango huo.

Mhe. Dkt. Mwanjelwa amesema, serikali inahitaji utaalam wa watumishi wa umma katika kujenga utumishi wa umma imara uliotukuka, utumishi ambao utaziwezesha taasisi za umma zote nchini kutoa huduma stahiki kwa wananchi.

Mhe. Dkt. Mwanjelwa amesisitiza kuwa, hategemei kumuona mtumishi wa umma yeyote akijihusisha na siasa zinazosababisha kukwamisha azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuwahudumia wananchi wake kikamilifu.

Aidha, Mhe. Dkt. Mwanjelwa amewataka Makatibu Tawala wa Mikoa kuwasimamia kikamilifu Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri ili kujenga ushirikiano wa kiutendaji kati ya Makatibu Tawala wa Wilaya  na Wakuu wa Wilaya kwa lengo la kuboresha utoaji huduma bora kwa umma.

Mhe. Dkt. Mwanjelwa amehimiza ushirikiano wa watendaji hao ili kurahisisha utendaji kazi wa shughuli za serikali kwa ujumla, na kuongeza kuwa, serikali iliyopo madarakani ni moja tu inayoongozwa na Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, hivyo anashangaa inakuwaje Makatibu Tawala wa Wilaya wasiarifiwe masuala yanayoendelea katika halmashauri.

“Kuanzia sasa barua yoyote ya kiutendaji itakayotoka mkoani kuelekezwa kwa Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri, ni lazima nakala ya barua hiyo ielekezwe pia kwa Makatibu Tawala wa Wilaya ili wafahamu kinachoendelea na kumuarifu Mkuu wa Wilaya kufanya ufuatiliaji wa utendaji kazi’, amesisitiza Dkt. Mwanjelwa.

Mhe. Dkt. Mwanjelwa ameyasisitiza yote hayo wilayani Kisarawe ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kikazi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma Mkoani Pwani ambapo mpaka hivi sasa ameshakutana na watumishi katika Halmashauri ya Mji Kibaha, Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze na Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe.

Waziri Mhagama; Vijana Tumieni Fursa Zilizopo Nchini Kuanzisha Vijiwe Vya Kiuchumi

Na; OWM (KVAU) - SONGWE
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amewataka vijana nchini kuchangamkia fursa zilizopo kwenye maeneo yao kwa kuanzisha vijiwe vya kiuchumi.

Kauli hiyo ameitoa na Waziri Mhagama wakati akiwa kwenye ziara ya kukagua maendeleo na miradi ya vijana iliyopo katika Kituo cha Maendeleo ya Vijana, Sasanda kilichopo Kata ya Nyimbili, Mkoani Songwe.

Akiwa katika ziara hiyo Mhe. Mhagama alieleza kuwa, Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe. Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli imeendelea kutimiza azima yake ya ujenzi wa uchumi wa viwanda, hivyo vijana watumie fursa hiyo kujifunza mambo muhimu na kuanzisha viwanda vidogo vidogo ambavyo vitawafanya wabadilishe vijiwe wanavyokaa kuwa vya kiuchumi.

“Tunataka kuona vijana watakapo jifunza kilimo bora, ufugaji wa ng’ombe au nyuki wataweza kuboresha thamani mazao na bidhaa kwa kuanzisha viwanda vidogo ndani ya Mkoa wa Songwe, mkakati wetu katika kituo hiki ni kutoa mafunzo yatakayowawezesha vijana kuongeza thamani ya mazao na bidhaa watakazozalisha ambazo zitakuwa ni kichocheo muhimu katika kufikia maendeleo yao” alisema Mhagama

Aliongeza kuwa, Takribani vijana 500 kwenye kituo hicho wamejifunza stadi za maisha, ufundi na elimu mbalimbali zinazotolewa kwenye kituo ambazo zitawawezesha kujipatia kipato.

Sambamba na hilo, Mhe. Mhagama aliwahimiza Viongozi wa Mkoa kushirikiana na Ofisi yake ili waweze kuwasaidia vijana ambao wamekwisha anzisha viwanda vidogo vidogo ndani ya mkoa huo kwa kuwawezesha kuzalisha bidhaa zenye ubora na kuwatafutia soko la uhakika ndani na nje ya nchi.

Aidha, Waziri Mhagama alitoa rai kwa vijana kujiunga kwenye vikundi ambavyo ni endelevu na vyenye muelekeo  wa kuanzisha viwanda  vidogo vitakavyowawezesha kujiajiri na kuajiri wenzao na pelekea kufikia uchumi wa kati kama mpango wa maendeleo wa taifa unavyoelekeza.

Pia, aliwaelezea juu ya uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru ambazo zitafanyika katika Mkoa huo na kuwataka vijana na wanawake kutumia fursa hiyo kuutangaza vyema mkoa wa Songwe.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Vijana, Bw. James Kajugusi alieleza kuwa kituo cha Maendeleo ya Vijana cha Sasanda kimewawezesha vijana kujitambua na kujiwekea malengo ya maisha na kuyatekeleza kwa faida yao, jamii na taifa kwa ujumla.

“Tunatarajia kuanzisha mafunzo na programu zitakazowaelekeza vijana masuala ya kilimo biashara ambacho kitasaidia upatikanaji wa malighafi zitakazokuwa zinahitajika kwenye viwanda vilivyopo nchini,” alisema Kajugusi

Naye Bw. Silia Kibona ambaye ni mnufaika kupitia kituo hicho, aliishukuru Serikali kwa kuwajengea mazingira ya kujifunzia ambayo yamewasaidia kupata mafunzo muhimu na aliwahamasisha vijana wenzie kuhudhuria mafunzo yanayotolewa kwenye kituo hicho.

Kituo cha Maendeleo ya Vijana – Sasanda kilianzishwa mwaka 1979 kwa ushirikiano wa Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni wa Taifa, Vijana na Michezo iliyopo wakati huo pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya. Uanzishaji wa Kituo hicho ulifuatia kuanzishwa kwa mpango wa kuunda vikundi vya vijana vya uzalishaji mali, uliolenga kuwawezesha vijana wasio na ajira kuweza kujiunga na kufanya kazi za kujitegemea hasa katika sekta ya kilimo.

MWISHO
Powered by Blogger.

Report Abuse

About Me

TAARIFA MPYA KUHUSU APP YETU KAMA BADO HUPATI HABARI ZETU

Habari!! Ni kipindi cha takribani wiki 1 kimepita ukiwa hupati habari, tunaomba radhi kwasababu tumekuwa tukifanya maboresho zaidi. Leo ...

Total Pageviews

Search This Blog

Blog Archive

Labels

Mobile Logo Settings

Mobile Logo Settings
image
recent/hot-posts

Random Posts

3/random/post-list

Recent Posts

3/recent/post-list