Kiongozi huyo amepoteza maisha nchini Afrika Kusini alikokuwa anapatiwa matibabu. Taarifa za kifo hicho zilianza kusambaa majira ya saa 12 jioni baada ya kifo chake kutokea saa 10:30
Ruge kwa muda mrefu alikuwa anasumbuliwa na maradhi ya figo hadi alipopatwa na umauti.
Alikuwa mmoja kati ya watu walioupigania muziki wa Bongo Fleva hadi kufikia hapo ulipo kwa sasa, hivyo wasanii mbalimbali wameoneshwa jinsi walivyoguswa na msiba huo mzito.
Elias Barnaba
Huyu ni mmoja kati ya wasanii ambao wameguswa na kifo cha mkurugenzi huyo. Kupitia ukurasa wake wa Instagram, aliandika:
“Tazama hapa mzee baba amka, Ruge jamani moyo wangu mbovu jamani baba sitaki, amka Mungu wangu jamani, baba naumia jamani, naumia hapana baba nimekuimbia wimbo jana nikaomba angalau utumiwe usikie baba sasa wee moyo wangu hauna nguvu tena,” aliandika hivyo.
Barnaba ni mmoja kati ya wasanii ambao wamepata umaarufu kupitia kwa Ruge, msanii huyo alikuwa mmoja kati ya zao la Tanzania House of Talent (THT) ambayo ilianzishwa na Ruge.
Mwasiti Almasi
Ukizungumzia mazao ya THT, huwezi kuliacha jina la Mwasiti Almasi, alikuwa mmoja kati ya wasanii waliotangazwa na kituo hicho kwa wasanii wa kwanza kabisa kutambulika na muziki wa Bongo Fleva.
Yeye ni mmoja kati ya wasanii walioshindwa kuzuia hisia zake hasa pale alipokuwa anahojiwa na kujikuta akitokwa na machozi mara zote.
“Mungu wangu hili tabasamu hatulioni tena, uwii dah inaumiza sana, Ruge aliwahi kuniambia, Mwasiti nawapenda sana wadogo zangu mkitimiza ndoto zenu ndio faraja yangu, daa umeenda boss Ruge jamani umeenda boss jamani uwii siamini,” aliandika hivyo kwenye ukurasa wake wa Instagram.
Ambwene Yesaya ‘Ay’
Ni mmoja kati ya wasanii wanaoamini kuwa Ruge alikuwa na mchango mkubwa katika tasnia ya burudani nchini, hivyo kwenye ukurasa wake wa Instagram aliandika: “Pumzika kwa amani kaka yetu Ruge Mutahaba, tutakukumbuka kwa mengi uliyofanya poleni sana Clouds FM, Cloud TV ndugu jamaa na marafiki.”
Mwana FA
Kutokana na kuguswa sana na kifo hicho, Hamis Mwinjuma hakuwa na mengi ya kuandika kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii, aliposti picha ya moyo ukiwa umechanika na kuandika neno Ruge.
Maneno mafupi kama vile Pumzika Pema Peponi Bosi Ruge Mutahaba, yaliandikwa na wasanii mbalimbali ikiwa pamoja na Joseph Haule maarufu kwa jina la Professor Jay. Upande wake msanii Aslay Isihaka aliandika kwa kifupi: “Mungu akupe kauli thabeet father huko uendapo.”
Nikki wa Pili
Rapa kutoka kundi la Weusi, Nickson Simon, ni mmoja kati ya wasanii waliotumia kwa upana sana ukurasa wao wa Instagram kwa kuandika yale ya moyoni baada ya kupata taarifa ya kifo hicho.
“Tunachonga barabara kamata fursa, tunakufungulia dunia, hayo yote yanamaanisha wengi wanakumbuka kwa kuwapa njia.
“Lakini nini maana ya njia? uliamini njia huanza kwa kukata msitu na kupasua milima hivyo endelevu, lazima kuhusisha kijiji hadi mkoa, barabara moja mpaka njia nne, njia isiyoendelea hupitwa na wakati, njia huboa baadhi ya vijiji, njia hupata lawama lakini ndio iletayo maendeleo, njia hubeba walio wema na wabaya, misiba na harusi, njia hupiganiwa ndio maana kuna mistari ili kupunguza ugomvi lakini ajali hutokea.
“Njia si mali yako unaweza pitwa na yeyote ukaporwa kijiti na njia kuu ni lazima utaiacha, kumbuka kutengeneza njia ya kwenda bomani kwako hivyo lazima kupambana, R.I.P Genius,” aliandika Nikki.
Amini
Ni miongoni mwa zao la THT, hivyo msanii huyo alipofanya mazungumzo na mwandishi wa makala haya, alisema kwa kushirikiana na wasanii wenzake waliotokea kwenye kundi hilo, watahakikisha wanaifanya THT iendelee kuishi kama alivyopanga Ruge.
Kala Pina
Amedai ataendelea kumkumbuka Ruge kwa kuwa alimpa wazo la kuanzisha kipindi cha Dawa za Kulevya kupitia Clouds TV.
“Nitaendelea kumkumbuka Ruge kwa kuwa wazo la kipindi ambacho alinipa kiliweza kusaidia kuwabadilisha vijana kwa namna tofauti huku wengine wakiacha kabisa kutumia dawa za kulevya,” alisema Kala Pina.
Alisema wazo la kuanzisha kipindi hicho lilitoka kwa Ruge, atamkumbuka Ruge kupitia kipindi hicho kwa kuwa aliweza kusababisha watu kuacha dawa za kulevya.
Kala Jeremiah
Msanii huyo amedai kwamba, mwaka 2017 aliitwa na Ruge na kumshauri namna ya kufanya muziki wake ili kuweza kuwafikia vizuri mashabiki wake.
Hata hivyo, katika mazungumzo hayo, alimwambia kuna kitu ambacho watakuja kukifanya, lakini kwa bahati mbaya hadi anapoteza maisha juzi hawajaweza kufanya lolote.
Steve Nyerere
Amewataka wasanii na wadau mbalimbali nchini kumsamehe Ruge Mutahaba kama waliwahi kukosewa na mwasisi huyo wa THT.
“Binadamu tujifunze kusamehe, najua wapo watu ambao walikosewa na Ruge, hivyo wanatakiwa kusamehe na wale wote ambao wanatumia mitandao ya kijamii kwa kuandika maneno ya kejeli juu ya Ruge ni vizuri wakachukuliwa hatua, ili ni pigo kubwa kwa wasanii wote hadi wa filamu kwa kuwa alikuwa na mchango sehemu zote,” alisema Steve.
Mr Blue
Yeye aliandika: “Pumzika kwa amani kaka yetu kipenzi, Ruge Mutahaba Mungu kakupenda zaidi.”
Wakati huo huo, Zuwena Mohamed maarufu kwa jina la Shilole, aliandika: “Kwa hiyo sikuoni tena na tabasamu lako jamani Ruge, Mungu akupokee baba yetu umeacha pengo kubwa sana kwa wengi wenye upendo wa kweli na wewe kwenye tasnia tunalia, nani atatusaidia tena saini ya kwenda America na sehemu zingine, kila nafsi itaonja umauti.”
Kwa mujibu wa msemaji wa familia ya Ruge, Anneck Kashasha, mwili wa marehemu utaingia kesho Ijumaa na kuagwa Jumamosi kwenye Ukumbi wa Karimjee na kusafirishwa Jumapili kuelekea Kagera na mazishi yatafanyika Jumatatu.
No comments:
Post a Comment