Imewekwa Tar.: February 28th, 2019
Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania imetoa fursa ya ajira zaidi ya elfu nne kwa Walimu wa Shule za Msingi na Sekondari ili kupunguza changamoto ya uhaba wa walimu mashuleni nchini.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(OR-TAMISEMI) Mhe.Selemani Jafo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Reform uliopo katika ofisi za OR - TAMISEMI Jijini Dodoma.
Mhe. Jafo amesema kuwa sasa ni wakati wa walimu wenye sifa kuchangamkia fursa ya ajira kwa kutuma maombi yao kwa njia ya mtandao kupitia kiunganishi mtandao cha http://ajira.tamisemi.go.tz (Online Teacher Employment Application System-OTEAS).
“Muombaji awetayari kufanya kazi sehemu yoyote kwani sisi tutapanga kulingana na maeneo yenye uhitaji wa walimu wenye sifa husika katika maeneo hayo kwani sisi ndio tunajua wapi kuna upungufu wa walimu” ameeleza Mhe.Jafo
Mhe.Jafo ametoa wito kwa waombaji wote watakaopata nafasi hizo kwenda kufanya kazi kwa moyo mmoja na weledi wa juu ili kuhakikisha watanzania wananufaika na elimu inayotolewa na wao, na hapo changamoto ya uhaba wa walimu katika sekta ya elimu itakuwa imetatuliwa.
Aidha, Mhe. Jafo amesema Walimu wanaotakiwa kutuma maombi ni wenye sifa za kitaaluma, Walimu wa Shule za msingi Daraja la IIIA wenye Astashahada ya Ualimu, Walimu Daraja la IIIB wenye Stashahada (Diploma) ya Ualimu katika masomo ya Kiingereza, Uraia, Historia, Jiografia na Kiswahili.
Walimu wa Daraja la IIIC wenye Shahada ya Ualimu kwa masomo ya Kiingereza, Uraia, Maarifa ya Jumla (General Studies), Historia, Jiografia na Kiswahili.
Huku sifa nyingine ya walimu wa shule za msingi ikiwa ni mwalimu wa Daraja la IIIC wenye Mahitaji Maalum aliyehitimu shahada ya ualimu kwa masomo ya Englishi, Civics, General studies, history, Jeiography na Kiswahili.
Huku sifa za walimu wa shule za Sekondari ni walimu wa Daraja la IIIC wenye shahada ya ualimu waliosomea elimu maalum, Walimu Daraja la IIIB wenye shahada (Diploma) ya Ualimu waliosomea elimu maalum, walimu wa Daraja IIIB wenye shahada, Daraja la IIIC katika masomo ya Sayansi ya Kilimo, Uchumi wa Nyumbani (Home Economics), Fizikia, Hisabati, Kemia na Biolojia.
Mhe. Jafo ameongezea kuwa sifa za jumla kwa waombaji ni sharti awe mtanzania, awe amehitimu kati ya mwaka 2014 hadi 2017 isipokuwa kundi maalum la wahitimu wa Elimu ya Ualimu wa masomo ya Fizikia na Hisabati hawa hawana muda maalum wa kuhitimu, lakini asiwe na umri wa miaka 45 wakati anatuma maombi na walimu waliowahi kuomba na hawakupata nafasi, wanapaswa kutuma maombi upya.
Amehitimisha kwa kusema barua zote za maombi ziambatishwe na nakala ya vyeti vya taaluma, utaalamu na kuzaliwa ambapo mwisho wa kupokea maombi hayo ni tarehe 15 mwezi Machi, 2019.
No comments:
Post a Comment