Serikali imekisia kuandikisha wapigakura wapya milioni nne kabla ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2020.
Kauli hiyo imetolewa leo Alhamisi Januari 31,2019 na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira na wenye Ulemavu, Anthony Mavunde alipokuwa akijibu swali bungeni mjini Dodoma.
Mavunde alikuwa anajibu swali la nyongeza la mbunge wa viti maalumu (Chadema), Cecilia Pareso ambaye ametaka kujua ni namna gani katika kipindi kilichobaki Serikali inaweza kutoa haki kwa Watanzania wenye sifa kujiandikisha ili watumie haki yao mwakani kupiga kura.
Katika swali la msingi, mbunge huyo amehoji ni lini Serikali itaanza mchakato wa kuboresha daftari la wapiga kura.
Akijibu, Mavunde amesema: "Mheshimiwa Spika, mchakato wa kuboresha daftari la wapigakura ulianza mwezi Agosti 2018, kwa kuhuisha kanzidata ya daftari la kudumu la wapigakura na kuboresha mifumo ya uandikishaji na utunzaji wa kumbukumbu za daftari."
Mavunde amesema kwa mujibu wa kifungu cha 15(5) cha Sheria ya Uchaguzi, sura ya 343, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) iko katika hatua za mwisho za kufanya maandalizi ya uboreshaji wa daftari kwa majaribio katika baadhi ya mikoa.
Mwaka 2015, Watanzania 22,751,292 waliandikishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na 503,193 waliandikishwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).
Katika uchaguzi huo jumla wagombea 1,218 wa nafasi za ubunge waliteuliwa, kati yao wanaume walikuwa ni 985 na wanawake 233.
No comments:
Post a Comment