Wabunge wameitaka Serikali kuangalia upya adhabu zilizowekwa katika Muswada wa Sheria ya Maji na Usafi wa Mazingira, ikiwemo mtu atakayepatikana kwa kosa la matumizi ya mabaya ya maji kutozwa faini ya kati ya Sh5milioni hadi Sh10 milioni.
Akiwasilisha maoni ya kambi ya upinzani bungeni leo Januari 31 mwaka 2019, msemaji wa kambi hiyo, Hamidu Bobali amesema faini zilizowekwa katika makosa hayo ni kubwa ukilinganisha na uzito wa kosa ambalo lingehitaji tu kuelimishwa.
“Katika makosa yaliyotajwa pamoja na kosa la kutumia maji vibaya chini kifungu cha 63. Kifungu hiki hakijaeleza maana ya matumizi mabaya ya maji. Kifungu hiki kinaweza kuwaweka wananchi wengi matatani pale kitakapotumika vibaya,” amesema.
Amesema kifungu cha 65 cha muswada huo kinaozungumzia makosa ya kutumia maji kinyume na matumizi yaliyoainishwa ambapo adhabu imeainishwa kuwa faini ya kiasi cha Sh5milioni au kifungo kisichopungua miezi sita.
Pia amesema kifungu cha 66 cha muswada huo kimebainisha kuwa adhabu kwa makosa kama ya kuosha au kufua na kuoga na kusababisha au kuruhusu kitu kuingia kwenye miundombinu ya maji ni faini ya Sh 50,000 au isiyozidi Sh 1milioni au kifungo cha mwezi mmoja.
No comments:
Post a Comment