Klabu ya Chelsea Jumatano usiku imekubali kipigo kizito cha goli nne bila majibu kutoka kwa klabu ya Bournemouth. Kipigo hicho ni kikubwa zaidi kwa Chelsea kwa kipindi cha miaka 23 kwenye Ligi ya Premia. Kipigo kikubwa cha ‘mbwa koko’ ambacho Chelsea ilipokea ilikuwa Septemba 1996 walipofungwa 5-1 dhidi ya Liverpool.
Mpaka mapumziko kulikwa hakuna goli lililofungwa. Kipa wa Bournemouth Artur Boruc alikuwa nyota wa mchezo katika kipindi cha kwanza kwa kuzuia nafasi za wazi tano za Chelsea.
Gharika langoni mwa Chelsea ilianza dakika mbili tu baada ya mapumziko kwa Joshua King kuandika goli la kwanza katitika dakika ya 47.
King alikuwa mwiba mchungu kwa safu ya ulinzi ya Chelsea kwa kutengeneza goli la pili lililofungwa na David Brooks katika dakika ya 63. Goli la tatu lilifungwa na King katika dakika ya 74 kabla ya Charlie Daniels kupigilia msumari wa mwisho katika jeneza la Chelsea katika dakika za majeruhi (90+5).
Kipigo hicho kimewashusha Chelsea mpaka nafasi ya tano wakiwa sawa na Arsenal kwa alama 47 lakini Gunners wapo nafasi ya nne kwa kuwa wamefunga magoli mengi kuliko Blues.
Ushindi wa Bournemouth unaifaya klabu hiyo kupaa mpaka nafasi ya 10 kwenye msimao wa ligi na kufikisha alama 33.
Kocha wa Chelsea Maurizio Sarri amesema anabeba lawama zote baada ya kikosi chake kukubali kipigo hicho kizito.
Sarri amesema wachezaji wake hawakucheza kama timu kipindi cha pili na walikuwa wazito kukubali kutanguliwa.
“Labda sina uwezo wa kuwafanya wawe na ari ya kujituma wachezaji hawa,” amesema kocha huyo raia wa Italia.
“Wakati tunaenda mapumziko ilikuwa ni vigumu kufikiria kuwa kipindi cha pili kingeikuwa majanga na nitaka kujua kwa nini imekuwa hivyo … kama miezi miwili iliyopita tulikuwa tukicheza kama watu 11 tofauti na si timu moja. Nilifikiri hali hiyo ilibadilika tulipowafunga Tottenham wiki iliyopita, lakini bado. Kuna kitu lazima kibadilike.”
Chelsea walianza msimu kwa kutofungwa katika michezo 12 lakini sasa wameshapoteza michezo minne kati ya 12 waliyocheza hivi karibuni.
Kwa Upande wa Majogoo, Liverpool nao wamepoteza nafasi ya kutanua pengo kati yake na Mnchester City kileleni mwa Ligi ya Premia kwa alama saba baada ya kukubali sare ya 1-1 dhidi ya Leicester City.
Sadio Mane aliwatanguliza Majogoo wa Jiji Liverpool katika dakika ya tatu ya mchezo lakini goli hilo lilisawazishwa na Harry Maguire mwishoni kabisa mwa kipindi cha kwanza (dakika ya 45+2).
Laiti Liverpool inelipata ushindi, wangelifikisha alama 63 na kuwaacha mbali City wenye alama 56 baada ya kufungwa na Newcastle Jumanne usiku.
Sasa Liverpool wameongeza wigo wa uongozi kwa alama moja na kufikisha alama 61 na kufanya tofauti yao na City kuwa alama 5.
Kocha wa Liverpool Mjerumani Jurgen Klopp amelaumu theluji zilizodondoka wanjani Anfield zimechangia pakubwa timu yake kutokuwa na mchezo mzuri na kufanya wapate matokeo ya sare.
“Umeona mpira ulikuwa hauendi kwa kasi kabisa … na kama unamiliki mpira kwa asilimia 70 mpaka 80 basi mabo ndio yanakuwa magumu kabisa,” amesema Klopp.
Liverpool hata hivyo walinyimwa mkwaju wa penati baada ya Naby Keita kuchezewa faulo na Ricardo Pereira katika eneo la hatari.
No comments:
Post a Comment