Watu wanne wamekufa papo hapo na wengine 7 kujeruhiwa baada ya kupigwa na radi wakiwa kilabuni wakinywa pombe katika kitongoji cha Nkata kijiji cha Kate, Nkasi mkoani Rukwa.
Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kate, Amesema kuwa watu hao walikuwa wanakunywa pombe katika kilabu hicho, ghafla ilipiga radi katika eneo hilo, hali iliyosababisha watu wengi kuanguka na kupoteza fahamu.
Baada ya kuwafanyia uchunguzi watu hao waliokuwa katika kilabu hicho, Mwenyekiti amesema ilibainika wanne kati yao wamefariki dunia papo hapo na wengine kujeruhiwa na kupelekwa kwenye zahanati ya Kanisa Katoliki iliyoko kijijini hapo. Ambapo baada ya kufikisha hapo kwa huduma, wengine walizinduka na kuruhusiwa kurudi nyumbani.
Mwenyekiti huyo aliwataja waliofariki dunia kuwa ni John Sumuni (31), Akleo Feluzi (45), Boniface Fundililwa (38) na Anastazia Njali (48) wote wakazi wa kijiji hicho.
Naye, Mganga Mfawidhi wa zahanati ya Kate Mission, Elly Joseph, alikiri kuwapokea majeruhi zaidi ya 10 na baada ya kuwapatia huduma ya kwanza, wengi wao waliruhusiwa kurudi nyumbani na wanne waliokuwa mahututi walibaki na wanaendelea na matibabu.
Tayari Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Said Mtanda, amekiri kutokea kwa tukio hilo na kuthibitisha kuwa watu wanne ndio waliopoteza maisha na kuwa wako kwenye kikao baada ya hapo yeye na viongozi wenzake watakwenda katika kijiji hicho kuwajulia hali majeruhi na kushiriki mazishi ya watu waliopoteza maisha.
Chanzo: Nipashe
No comments:
Post a Comment