Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda amejipa cheo kipya cha umeneja wa miradi wa mkoa huo, baada ya kukuta mradi wa ujenzi wa mto Ng'ombe wilayani Kinondoni kusimama, licha ya viongozi wa wilaya hiyo kumdanganya kuwa Mkandarasi yupo 'Site'.
Hayo yamejiri leo Oktoba 1, 2019 alipofanya ziara ya kukagua miradi ya maendeleo wilayani humo, ambapo akiwa katika mradi wa maboresho ya Mto Ng'ombe unaogharimu Shilingi Bilioni 32 ukiwa na urefu wa Km 7.5 ndipo alipobaini kuwa alifanyiwa mchezo mchafu na viongozi hao.
''Mimi ni meneja mkuu wa miradi ya mkoa wa DSM, hiki ni cheo kipya cha mwezi wa kumi na nimekipata baada ya kuona mambo hayaendi tunavyotegemea, ukibaki na cheo cha ukuu wa mkoa utabaki kupokea taarifa ofisini, lakini ukiwa meneja miradi, utatembelea mradi wako kuanzia unajengwa hadi unakamilika'', amesema Makonda.
Kufuatia hali hiyo Makonda amewaonya watendaji wanaoendelea kumpa taarifa za uongo na kwamba yeye bado ataendelea kufanya ziara kwenye kila mradi ili kujionea kama taarifa anazoletewa kwenye karatasi zinaendana na kinachofanyika.
Akiwa kwenye mradi wa ujenzi wa Soko la Kisasa la Magomeni linalogharimu kiasi cha Shilingi bilioni 8.9, Makonda amemtaka mkandarasi kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha soko hilo linakabidhiwa Disemba mwaka huu.
No comments:
Post a Comment