Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amewaagiza wakandarasi kuacha tabia ya kuchelewa kuwaunganishia umeme wananchi.
Ametoa agizo hilo katika Kijiji cha Mwisi, Uswaya na Isenegeja wilayani Igunga mkoani Tabora ambapo aliwasha umeme katika Kijiji cha Isenegeja na kuwasisitiza wananchi kulipia gharama ya shilingi 27,000 tu, na bila kujali aina ya nyumba wanazomiliki.
“Umeme ndiyo nguzo kuu ya maendeleo, hivyo nawasisitiza kuchangamkia huduma hii inayotolewa na Serikali ili muweze kujifanyia shughuli mbalimbali za kiuchumi, kama tulivyosema umeme hautachagua nyumba, umeme wa Serikali hii unapelekwa kwa Watanzania wote bila kujali masikini, tajiri au Mtanzania wa kawaida.”amesema Dkt. Kalemani.
Aidha, Dkt. Kalemani amewaagiza wakandarasi kuacha tabia ya kuchelewa kuwaunganishia umeme wananchi.
”Nimeshasema ni marufuku kuchelewa kuunganishia umeme wananchi, mtu akishalipia muunganishie umeme ndani ya siku Saba bila kisingizio chochote.”amesisitiza
Kuhusu hali ya umeme nchini, amesema kuwa, hali ya umeme ni nzuri na endapo kunatokea kukatika kwa nishati hiyo, ni kwasababu ya hitilafu tena ya dharura ama kwasababu ya matengenezo.
Kwa nyakati tofauti wananchi wa Vijiji hivyo waliishukuru Serikali kwa kuona umuhimu wa kusambaza nishati ya umeme vijijini na kueleza kuwa itawawezesha kufanya shughuli mbali mbali ikiwemo kuanzisha mashine za kukoboa nafaka.
No comments:
Post a Comment