POLISI wameungana na klabu ya Manchester United kwenye msako wa kuwasaka wale wote walituma meseji za kumbagua kiungo Paul Pogba kulingana na rangi yake huko kwenye mtandano wa kijamii wa Twitter.
Pogba alijikuta kwenye wakati mgumu wa kuandikiwa meseji za kubaguliwa kwa ngozi yake na vitisho kwa sababu tu alikosa penalti kwenye mechi ya sare ya 1-1 dhidi ya Wolves kwenye Ligi Kuu England, Jumatatu iliyopita.
Na sasa polisi wa jiji la Manchester watafanya kazi bega kwa bega na klabu ya Man United kuwasaka wahusika na kuwapa adhabu kali kwa kuendekeza ubaguzi katika dunia ya sasa.
Wahusika wa mtandao wa Twitter wameshapanga kukutana na maofisa wa kampeni ya Kick It Out kupanga njia nzuri ya kuwakamua wale wote wenye tabia hizo za kufanya ubaguzi unaotokana na rangi ya mtu.
Wanasoka mbalimbali duniani wameonekana kupaza sauti zao kutokana na ubaguzi huo aliofanyiwa Pogba, huku staa wa zamani wa Man United na England, Phil Neville kudai kwamba pengine umefika wakati wa kuufungia mtandao wa Twitter kwa miezi sita.
Mitandao ya kijamii imeelezwa kwamba umefika wakati wa kuhakikisha wanatafuta namna ya kuwadhibiti watu wenye kawaida ya kufanya ubaguzi kwa maana ya kuwatambua na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria.
Straia, Marcus Rashford aliongeza: "Kwa kweli inatosha sasa, tunahitaji kulikomesha hili. Manchester United ni familia na Paul Pogba ni mmoja wa wanafamilia wakubwa kabisa. Mnapomshambulia, mmetushambia wote."Beki Harry Maguire aliandika: "Inachefua. Hii mitandao ya kijamii inapaswa kufanya kitu juu ya hili. Kila akaunti ya mtu iwe inathibitishwa kwa hati ya kusafiria au leseni ya udereva. Kwa jambo hilo litakomesha wingi wa kuwa na akaunti za mitandao hiyo ya kijamii."
No comments:
Post a Comment