Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera amesema wachezaji inapaswa watumie michezo ya kirafiki wanayocheza ili kuonyesha uwezo wapate nafasi kwenye kikosi cha kwanza
Akizungumza baada ya mchezo wa kirafiki dhidi ya Polisi Tanzania ambao ulimalizika kwa Yanga kufungwa mabao 2-0, Zahera alisema baadhi ya wachezaji itakuwa ngumu kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza
"Tulicheza michezo miwili ya kirafiki Zanzibar, mchezo wa kwanza timu moja iliyoanza iliingiza mabao matatu kwenye kipindi cha kwanza, tukabadili wote kwenye kipindi cha pili, walioingia wakafunga bao moja," Zahera aliiambia Azam TV
"Mchezo wa pili tukaitumia timu hiyohiyo, wakatoka sare ya 1-1. Leo tena tumewapa nafasi lakini tumepoteza"
"Baadhi ya wachezaji wanaonyesha uwezo na tunaweza kuwajumuisha kwenye kikosi cha kwanza lakini wengine itakuwa ngumu"
Aidha, pamoja na changamoto hiyo ya kikosi chake, Zahera amesema mazingira ya uwanja lilikuwa tatizo pia
"Wachezaji wetu wengi wanacheza mpira, sasa kwa hali ya uwanja huu ni ngumu kupiga pasi mbili au tatu"
Zahera amesema mchezo wa kesho dhidi ya AFC Leopards atatumia kikosi chake cha kwanza

No comments:
Post a Comment