Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mh. Paul Makonda, amewashangaa watu wanaohoji kitendo cha Rais Magufuli kukutana na watendaji wa kata, ambapo amesema kuwa wengi ambao wamekuwa wakihoji walishashindwa kutimiza majukumu yao kwa wananchi.
Makonda ameyabainisha hayo leo Agosti 31, 2019 wakati akizungumzia ujio wa ugeni ikiwa ni pamoja na kumpongeza Rais Magufuli kwa kuona umuhimu wa kukutana na viongozi hao wa ngazi ya chini.
“Dkt Magufuli alichokiamua hata akitaka kukutana na wenyeviti wa mitaa na penyewe mtasema wote anataka wahamie CCM, unajua shida moja tunaruhusu akili ndogo kujadili mambo makubwa, na sisi watanzania wengi tunapoteza sana muda kufikiria vitu kwa njia hasi'', amesema Makonda.
Aidha Makonda amewataka watendaji hao wanaokuja jijini humo kutokuwa na hofu ya kuibiwa mali zao, kwani jiji hilo kwa sasa halina wizi wa namna hiyo kama ambavyo watu wa mikoa mingine wamekuwa wakifikiria.
Rais Magufuli atakutana na watendaji wa Kata nchi nzima Ikulu ya Dar es Salaam siku ya Septemba 2, 2019.
No comments:
Post a Comment