Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera amesema anafahamu beki kisiki wa timu hiyo Kelvin Yondani alipewa mapumziko baada ya kumalizika kwa michuano ya Afcon hivyo atarejea kikosini baada ya kumaliza majukumu ya timu ya Taifa
Yondani anayepigiwa chapuo kupewa kitambaa cha unahodha, hakuripoti kambini mkoani Morogoro kuungana na kambi ya Yanga lakini juzi aliripoti kambi ya timu ya Taifa inayojiandaa na mchezo dhidi ya Kenya Julai 28
"Kelvin alipaswa kupumzika sababu ya Afcon na mapumziko yake yalimalizika wakati anaitwa timu ya Taifa, hivyo atarejea kikosini baada ya mchezo dhidi ya Kenya," amesema
Jana uongozi wa Yanga ulitarajiwa kuwajadili wachezaji ambao hawakuripoti kambini Morogoro akiwemo Yondani, Juma Abdul na Andrew Vicent
Asema haidai Yanga
Katika hatua nyingine kocha Mwinyi Zahera amewashukia wanaosambaza taarifa za uongo kuwa amegoma kurejea Yanga kwa kuwa anaidai timu hiyo
"Mimi kocha Zahera sidai hata elfu moja kwa Yanga. Hakuna siku nimelipa fedha kuingiza timu kambini kama wanavyosema, wala sijalipia ndege wala kitu chochote"
"Mimi nilisema kama Afcon itamalizika napaswa kwenda nyumbani kupumzika kwa angalau siku 15 kama ilivyokuwa kwa watu wote waliokuwa na majukumu na timu za Taifa Misri"

No comments:
Post a Comment