Aliyasema hayo jana Jumanne Julai 2, 2019 baada ya kukagua kiwanda cha ngozi cha ACE Leather Tanzania Ltd kilichopo mkoani Morogoro na baadaye kuzungumza na wadau wa bidhaa hizo.
Profesa Ole Gabriel amesema kuna malalamiko mengi kuhusu ngozi zinazozalishwa nchini kuwa zinaharibika kutokana na kukosa soko.
Hata hivyo, amesema malalamiko hayo yanaweza kumalizika kama ngozi itakayozalishwa hapa nchini itakuwa na ubora na itaongezewa thamani kwa kuichakata na kutengeneza bidhaa mbalimbali kama viatu, mikoba na mikanda.
Profesa Ole Gabriel ameutaka uongozi wa kiwanda hicho kuharakisha ufungaji wa mashine za kuongeza thamani ya ngozi kwa kuweka mapambo mbalimbali tofauti na ilivyokuwa sasa.
Naye Mkurugenzi mkuu wa kiwanda hicho, Onorato Garavaglia ametaja changamoto ya ubora wa ngozi kuwa unaanzia kwa mfugaji hasa wanapoweka alama kwenye mifugo yao.
Garavaglia ametaja changamoto nyingine kuwa ni matundu kwenye ngozi yanayotokana na uchunaji usiozingatia taratibu na hivyo kusababisha ngozi kukosa ubora unaotakiwa.
Akizungumzia mikakati ya kuongeza thamani ya ngozi, Garavaglia amesema mpaka ifikapo mwisho wa mwaka huu, kiwanda hicho kitakuwa kimefungwa mashine za kuweka rangi na mapambo mbalimbali kwenye ngozi.
Naye Kaimu mkurugenzi wa mazao ya mifugo, usalama wa chakula na lishe kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Gabriel Bura amesema katika kupunguza changamoto ya matundu kwenye ngozi, tayari walishawapa mafunzo wachanaji ngozi wa machinjio ya manispaa ya Morogoro wapatao 200.
Amesema baada ya kutoa mafunzo kwa sasa wanaandaa leseni kwa ajili ya kuwapa wachunaji hao ili kuifanya kazi hiyo iwe rasmi na kuwatambua wachunaji ambao wana mchango mkubwa wa kuboresha ama kuharibu ngozi.

No comments:
Post a Comment