Serikali nchini kenya kuanzia leo Jumatatu itaanza kuchunguza nyeti za wanaume ikiwa wametahiriwa, katika kaunti nne za eneo la Nyanza.
Wizara ya Afya nchini humo imesema uchunguzi huo unaoendeshwa na Shirika la Wanaume Kutahiri kwa Hiari (VMMC) unalenga kuimarisha vita dhidi ya maambukizi ya virusi vya ugonjwa hatari wa Ukimwi katika kaunti hizo.
Uchunguzi huo pia unalenga kufahamu idadi ya wanaume waliotahiriwa katika kaunti za Homa Bay, Kisumu, Siaya na Migori. Wakati wa uchunguzi huo wa miezi mitatu, wahudumu waliopokezwa mafunzo watakagua kibinafsi uume wa mwanaume iwapo anayechunguzwa atakubali na akikataa atajibu tu swali iwapo amepitia kisu cha ngariba au la.
Hata hivyo, mila na desturi za jamii huenda zikazuia baadhi ya wanaume kuhojiwa kuhusu iwapo wametahiriwa au la.
Huduma za VMMC zilianza kutolewa katika eneo la Nyanza mwaka wa 2008 kabla ya kueneza huduma hizo hadi maeneo mengine ya nchi.
Jukumu lake lilikuwa kusaidia kukabiliana na kusambaa kwa virusi vya Ukimwi katika Kaunti za Nyanza ambazo zimekuwa zikisajili zaidi ya asilimia 20 ya maambukizi. Utafiti unaonyesha tohara hupunguza maambukizi ya virusi vya ukimwi kwa asilimia 60.
Kulingana na Dkt Akeche, utafiti wa kuchunguza nyeti za wanaume Nyanza umefadhiliwa na serikali ya Marekani pamoja na Kituo cha Kudhibiti Magonjwa(CDC) na utasaidia kuamua iwapo rasilimali zaidi zitawekezwa katika kupambana na ugonjwa wa Ukimwi maeneo ya Nyanza.
Chanzo: Taifa Leo, Kenya
No comments:
Post a Comment