Klabu ya Chelsea imemtangaza Frank Lampard kuwa kocha wake mpya baada ya kusaini mkataba wa miaka mitatu kuionoa klabu hiyo.
Lampard, 41, anaondoka katika klabu anayoinoa kwa sasa Derby County kuchukua hatamu katika klabu ya Chelsea ambayo alikuwa ni mchezaji kinara kwa miaka 13.
Anarithi nafasi iliyoachwa wazi na Maurizio Sarri, ambaye ameondoka mwezi uliopita kwenda kujiunga na miamba ya Italia klabu ya Juventus.
Lampard ameiwakilisha Chelsea katika mechi 648 Chelsea, na kunyakua mataji 11 na timu hiyo.
Hata hivyo anaenda kuingoza Chelsea katika kipindi ambacho wamepigwa marufuku ya kufanya usajili katika madirisha mawili na chombo kinachosiamamia mchezo huo FIFA, lakini tayari wameshakata rufaa katika mahakama ya kimataifa ya usuluhishi wa masuala ya michezo.
CHELSEA
"Ninafuraha isiyo kifani kurejea Chelsea kama kocha mkuu," amesema Lampard.
"Kila mtu anajua mapenzi yangu kwa klabu hii na historia yangu hapa. Lakini, malengo yangu kwa sasa ni juu ya kazi hii mpya na kujipanga kwa msimu ujao."
"Nipo hapa kufanya kazi kwa bidii, na natamani kazi ianze mara moja."
Uteuzi wa Lampard unakuja siku tisa tangu klabu ya Derby ilipomruhusu kufanya mazungumzo na Chelsea. na siku 18 toka Sarri alipoondoka klabuni hapo.
Lampard anakuwa kocha wa 10 kuifundisha Chelsea toka klabu hiyo iliponunuliwa na Roman Abramovich 2003.
Mkurugenzi wa Chelsea Marina Granovskaia amesema Lampard amedhihirisha uwezo wake kwa kuiongoza Derby kukaribia kupanda Ligi ya Primia.
Ni moja kati ya makocha vijana wenye uwezo mkubwa kwa sasa," amesema na kuongeza, "Inatupa faraja kubwa kumkaribisha tena Chelsea. Frank anaijua vyema klabu hii.
Lampard ameondoka Derby na makocha wasaidizi wake wawili, Jody Morris na Chris Jones. Petr Cech ambaye alikuwa ni kipa wakati Lampard akiwa kiungo Chelsea ataungana nao akiwa kama Mkurugenzi wa Ufundi.

No comments:
Post a Comment