Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Zainab Chaula amewataka Makatibu Tawala nchini kuendelea kuzisimamia Hospitali za rufaa za mikoa ambazo kwa sasa zinasimamiwa na Wizara ya Afya.
Dkt. Chaula amesema hayo jana alipokutana na Makatibu Tawala kutoka Mikoa ya Tanzania Bara katika Kikao Kazi cha Viongozi wa Hospitali za Rufaa za Mikoa kinachoendela kufanyika katika ukumbi wa Chuo cha mipango Jijini Dodoma.
“Licha ya Hospitali hizi kuhamishiwa usimamizi kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) lakini bado zipo kwenye maeneo yenu, tunawategemea nyie Makatibu Tawala kuzisimamia hospitali hizi.” Amesema Dkt Chaula.
Dkt. Chaula amesema kuwa ni dhahiri lengo lilikuwa ni jema tuu kutoka kwa Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli, kwamba Hospitali zisimamiwe na Wizara ya Afya ili ziweze kuwa na mahusiano ya moja kwa moja na Wizara ya Afya ambayo ndiyo Wizara mama inayotunga Sera na Miongozo pamoja na kusimamia Wadau.
Naye Mwakilishi wa Makatibu Tawala wa Mikoa katika kikao hicho Bi. Zena Said amempongeza Katibu Mkuu Wizara ya Afya kwa kuandaa kikao hicho cha kihistoria ambacho hakijawahi kufanyika kabla.
“Hili ni jambo la busara, pamoja na kwamba hizi Hospitali zimeondolewa kwenye mamlaka za Tawala za Mikoa lakini bado kuna mambo mengi ambayo bado tunayafanya kwa niaba ya Wizara” amesema Bi. Zena.
Kikao hicho cha kihistoria kinafanyika kwa mara ya kwanza tangu kuhamishiwa kwa usimamizi wa Hospitali za Rufaa za Mikoa tarehe 25, Novemba 2017 ambacho kitakuwa endelevu kila mwaka huku kikiwakutanisha viongozi wa hospitali, Waganga wakuu wa Mikoa pamoja na watendaji na wadau wa Sekta ya Afya nchini.


No comments:
Post a Comment