Na Ahmad Mmow, Lindi
Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Lindi kimeitaka kamati ya siasa ya chama hicho ya kata ya Nachingwea, wilaya ya Lindi ijadili tuhuma za ubadhirifu wa fedha za viwanja zilizolipwa na wananchi.
Agizo hilo lilitolewa jana katika kata hiyo na mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo, Abdallah Madebe alipozungumza na wananchi wa kata hiyo kuhusu tuhuma zinazowakabili baadhi ya viongozi wa mitaa kukwapua fedha za wananchi waliochangia ili wapewe viwanja vya makazi.
Madebe alisema kamati ya siasa ya kata hiyo hainabudi kukutana na kujadili tuhuma hizo zenye sura ya kuwagombanisha wananchi na serikali. Ambapo mapendekezo yatakayo pendekezwa, yapelekwe kwenye ofisi ya chama hicho ya wilaya ya Lindi ili ichukue hatua kwa mujibu wa mapendekezo hayo.
Aliwaonya wananchi waache tabia ya kuwapa fedha za malipo ya aina yoyote wenyeviti wa serikali za mitaa. Bali wenye haki na mamlaka ya kukabidhiwa malipo ya serikali za mitaa ni watendaji wa mitaa.
Kwa upande wake ofisa wa Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa( TAKUKURU), Elizabeth Bulugu alisema taasisi hiyo ilipokea malalamiko kutoka kwa wananchi. Ilipofanya uchunguzi ilibaini kuwepo ubadhirifu wa fedha hizo.
Huku baadhi ya viongozi walikiri kujikopesha na nyingine hazikuwa na maelezo ya wapi zilikokwenda.
Awali baadhi ya wananchi kwenye mkutano huo uliofanyika katika viwanja vya Mlandege walisema walimpa fedha mwenyekiti wa serikali ya mtaa aliyetajwa kwa jina la Mussa Chimbuli kwa ajili ya kupatiwa viwanja.
Hata hivyo licha ya kupewa stakabadhi lakini hawajaoneshwa wala kupewa viwanja. Wananchi hao walisema mtendaji wa mtaa ambao mwenyekiti wake ni Chimbuli alipoulizwa kuhusu kupewa viwanja, waliambiwa kwamba majina yao yalikuwa hayaonekani kwenye orodha ya watu waliochangia ili wapewe viwanja.
No comments:
Post a Comment