Mwenyekiti wa Yanga Dk Mshindo Msolla amesema timu hiyo imekamilisha usajili wake kwa asilimia 100 ambapo wachezaji wote wa ndani na nje waliopendekezwa na kocha Mwinyi Zahera wamepatikana
Akizungumza na waandishi wa habari mapema leo, Dk Msolla amesema kazi iliyobaki kwa sasa ni kumtengenezea kocha mazingira mazuri ya kukiandaa kikosi chake kuelekea msimu mpya
Zahera atakuwa na kazi ya kuiandaa Yanga imara kabla ya Julai 27 ambapo siku hiyo itaonekana hadharani kwa mara ya kwanza kwenye tukio la kilele cha wiki ya Mwananchi
"Tarehe 27/07 tutakuwa na matukio matatu, moja ni kutambulisha jezi, pili kutambulisha wachezaji wapya na tatu ni tutakuwa na mchezo kimataifa wa kirafiki," alisema Dk Msolla
"Tumesajili kulingana na matakwa ya mwalimu, hata huko alipo lazima atakuwa anafuraha maana wachezaji wote wa nje na ndani aliokuwa akiwahitaji tumewapata"
"Tayari ametutumia program yake ya mazoezi siku tatu zilizopita, sasa tunaifanyia kazi ili tuhakikishe kikosi chetu kinapata maandalizi mazuri"
Hii ni habari njema kwa mashabiki na Wanachama wa Yanga ambao kwa takribani misimu miwili, walikosa furaha ya kweli kutoka kwa timu yao
Aidha kocha Zahera atakuwa na nafasi ya kuonyesha makali yake kwenye ukufunzi wa soka kwani msimu uliopita alifanikiwa sio kutokana na ubora wa timu
Msimu ujao atakuwa na kikosi alichokipendekeza mwenyewe
No comments:
Post a Comment