Na Thabit Hamidu,Zanzibar.
Wabunge na Wawakilishi wa Viti Maalum UWT Mkoa wa Mjini wameandaa Mafunzo maalumu ya kuwajengea uwezo viongozi wa ngazi ya Wadi hadi Mkoa UWT Mkoa wa Mjini.
Mafunzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni mjini Magharib Unguja.
Akifungua Mafunzo hayo Naibu katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk Abdallah Juma Saadala maaruf Mabodi aliwataka viongozi hao wa UWT kujipanga vizuri na kuhakikisha CCM inapata ushindi wa kihistoria katika uchaguzi Mkuu ifikapo mwaka 2020.
Dk.Mabodi alisema Wanawake wa CCM wanatakiwa kuwa Mstari wa mbele katika kuandaa Mazingira rafiki ya upatikanaji wa ushindi wa Chama Cha Mapinduzi katika Uchaguzi Mkuu ujao, kwa kuongeza Wanachama wapya na kuhakikisha wanaipigia kura nyingi CCM katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Alisema Wanawake wana historia kubwa na nzuri ya kufanikisha harakati za ushindi wa Chama na mikakati mbali mbali ya Ukombozi wa Nchi za Afrika.
Alieleza kwamba UWT pamoja na Jumuia zingine za CCM zinatakiwa kushirikiana pamoja katika kuandaa mazingira ya Ushindi katika Uchaguzi ujao ili kutimiza kwa vitendo kauli mbiu ya Umoja ni Ushindi ndani na nje ya CCM.
Akizungumzia Mafunzo hayo Naibu Katibu Mkuu huyo Dk.Mabodi,amesema Mafunzo ni jambo muhimu sana katika shughuli za Kisiasa kwani Viongozi na Watendaji wanajengewa uwezo wa masuala mbali mbali ili watekeleze majukumu yao kwa uhakika.
“Mafunzo haya yasiishie katika Ngazi ya Wadi tu bali yashuke mpaka ngazi za Matawi hadi Mashina kwa lengo la kuhakikisha Jeshi letu linakuwa na uwezo mkubwa wa kufanikisha Ushindi wa CCM Mwaka 2020.”alisema Dk.Mabodi.
No comments:
Post a Comment