Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeruhusu wazazi kutumia vitambulisho vyao kusajili laini za watoto wao wenye umri wa chini ya miaka 18.
Usajili huo unaofanyika kwa kutumia alama za vidole, unataka kila mwenye namba ya simu kusajili kwa kutumia kitambulisho cha Taifa kwa ajili ya kupata taarifa zake.
Kaimu Mkuu wa TCRA Kanda ya Mashariki, Mhandisi Jumanne Ikuje amesema kwa sasa hakuna kizuizi kinachomzuia mzazi kumsajilia mtoto wake namba ya simu.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma iliyofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja, Ikuja amesema ni muhimu kwa watumiaji wa simu kufanya usajili huo.
“Kwa watoto wenye umri chini ya miaka 18, wazazi wao wanaweza kuwasajilia kwa kutumia vitambulisho vyao, akifikisha umri wa kupata kitambulisho atabadilisha taarifa zake ila kwa sasa ni muhimu kusajili,”
Maadhimisho hayo yalizihusisha pia kampuni zote za simu ambazo zilikuwa zinatoa huduma ya usajili kwa wakazi wa jiji waliojitokeza uwanjani hapo.
Sanjari na hao, ulikuwepo pia uwakilishi wa ofisi ya Uhamiaji, polisi kitengo cha uhalifu wa mtandao pamoja na maofisa wa Nida waliokuwa wakiandikisha na kutoa namba za vitambulisho kwa ajili ya usajili.
Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano Nida, Thomas Nyakabwenge amesema kumekuwepo na mwitikio mkubwa wa watu wanaofuatilia vitambulisho vya Taifa, jambo linalowafanya kuongeza vituo vya utoaji wa huduma hiyo.
“Mwitikio umekuwa mkubwa sana baada ya usajili wa simu kuhitaji vitambulisho hivi na sisi tunajipanga kuhakikisha watanzania wote wanapata, tumeongeza vituo na wakati mwingine kuweka kambi maalum kwenye maeneo yenye uhitaji zaidi,”
“Vitambulisho hivi ni muhimu maana ili nchi iweze kwenda lazima uwatambue raia wako na njia ya kuwatambua ni hivi vitambulisho kwa hiyo wananchi wajitokeze kujisaji wawe navyo,” amesema Nyakabwenge

No comments:
Post a Comment