Klabu ya soka ya Singida United imetangaza kuwa itaanza kutangaza rasmi usajili wake leo Juni 30 kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania bara.
Kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, klabu hiyo imesema kuwa kunzia Juni 30, saa 6:00 mchana itakuwa ikitangaza mchezaji mmoja.
Mfumo huo umekuwa ukitumiwa na Simba katika usajili wa kujiandaa na msimu ujao, ambapo imekuwa ikitangaza wachezaji wake kila siku majira ya saa 7:00 mchana, na mpaka sasa imeshaongeza mikataba na wachezaji wa msimu uliopita pamoja na usajili mpya wa wachezaji watatu wa Kibrazil.
Wachezaji watatu wapya waliosajiliwa ni pamoja na beki Tairone Santos da Silva (30) aliyetia saini ya miaka 2 akitokea Atlético Cearense FC ya nchini kwao Brazil, mwingine ni beki wa kati na kiungo mkabaji, Gerson Fraga Vieira (26) ambaye amesaini mkataba wa miaka 2 akitokea klabu ya ATK FC ya India pamoja na mshambuliaji Wilker Henrique da Silva ambaye amesaini mkataba wa miaka 2.
Singida United pia imetangaza tarehe ya kuanza kambi rasmi ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu kesho Julai 1, ambapo kambi hiyo itafanyika mjini Singida.
No comments:
Post a Comment