Amesema hawatapata nafasi ya kugombea kwa sababu taarifa zao zinakusanywa kupitia kamati ndogo ya usalama na maadili ya chama hicho tawala.
Polepole ametoa kauli hiyo jana mkoani Mtwara katika mahafali ya vyuo vikuu kwa wahitimu wa tawi la umoja la vijana ndani ya Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Mtwara.
Licha ya kutowataja majina, mbunge wa Mtama, Nape Nnauye na Hawa Ghasia wa Mtwara Vijijini, Juni 24 mwaka jana walieleza kutokubaliana na mapendekezo ya Serikali ya kufuta ushuru wa asilimia 65 wa fedha zinazotokana na mauzo ya korosho nje na kubainisha kuwa kinachofanywa ni kuiua CCM mikoa ya Kusini.
Aliyeanza kuzungumza alikuwa Nape aliyebainisha kuwa ukizungumzia korosho unazungumzia maisha ya watu mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Pwani na mingine inayolima korosho.
Wakati Nape akieleza hayo, Ghasia ambaye wakati huo alikuwa mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti alisema kuna wabunge wamekaa vikao na kuandaliwa kwa ajili ya kuwadhalilisha wabunge wanaotetea wakulima, akibainisha kuwa wawakilishi wote wa wananchi wana haki sawa, akitaka anayetoka katika pamba, madini atetee eneo lake kama ilivyo kwa wanaotokea katika korosho.
Nape, Ghasia wazungumza
Walipoulizwa kuhusu kauli hiyo ya Polepole, Ghasia alisema hawezi kuzungumza chochote kwa kuwa kiongozi wake ameshatamka
“Yeye ndio katamka hivyo mimi siwezi kubishana na kiongozi wangu, yeye katamka kwa hiyo sina lolote la kuzungumza,”alisema Ghasia
Kwa upande wake Nape alisema hawezi kuzungumza chochote hadi atakaposikia kauli ya Polepole, “Mpaka mimi mwenyewe nimsikie siwezi kujibu unachoniambia wewe.”
Maelezo zaidi ya Polepole
Katika ufafanuzi wake wa jana, Polepole alisema lazima wabunge hao wafahamu katika michakato (wa kutaka majina) naye anahusika na hata ukataji wake ni wa viwango.
Alisema wanaofanya hivyo wanapaswa kujipanga mapema kwa sababu yeye na sekretarieti ni kitu kimoja na kwamba Serikali iliweka mustakabali sawa kulinda utu na heshima ya wakulima kwa kununua korosho ili kulinda utu na heshima ya wakulima.
“Kama wewe ni mbunge wa CCM na unashiriki kuendeleza nongwa kwa jambo hili ambalo tumelifanya kwa uchungu mkubwa jipange mapema kwa sababu mimi na wenzangu kuanzia sekretarieti, kamati kuu na halmashauri kuu tupo kitu kimoja,” alisema Polepole.
Alisema wameweka mustakabaili sawa kulinda utii na heshima kwa mkulima kwa kununua korosho na kuhoji, “Hivi mtu anapoonewa na kusaidiwa huwa unahoji itakuwaje au atapaswa kupewa msaada kwanza?”
“Unamsaidia kwanza akishasaidika ndipo mtazungumza baadaye, sio unasema tunanunua halafu itakuwaje, nunua kwanza heshima ya watu isimame, ndoa za watu ziimarike, hapa watu wasingekuwa wamenunuliwa korosho zao tungekuwa tumeharibu uchumi mzima wa eneo hili.”
Mei 20, 2019 sakata la korosho liliwasha moto kwa mara nyingine bungeni huku wabunge watatu wakiikalia kooni Serikali na kuitaka kutoa majibu yatakayowaridhisha juu ya mchakato mzima wa uuzwaji wa zao hilo nchini.
Wabunge hao walisema hayo wakati wakichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka wa Fedha 2019/2020.
Nape alianza kwa kuchangia hoja juu ya zao hilo akiwataka waliohusika kulihujumu wawajibike wenyewe na wasipofanya hivyo, atapeleka bungeni kusudio la kuwataja mmojammoja.
Nape alisema Rais John Magufuli alikuwa na nia njema lakini waliokwenda kutekeleza mchakato mzima wa ununuzi walikwenda kuua zao hilo.
Katibu huyo wa zamani wa itikadi na uenezi CCM, pia alipendekeza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), akague na kupeleka ripoti bungeni jinsi kazi hiyo ilivyofanyika huku akidai iligubikwa na rushwa.
Polepole, pia aligusia bodi ya mazao mchanganyiko kuhakikisha pembejeo zinakuwa tayari na kwamba endapo itachelewa ataieleza Serikali kula vichwa vya watu kwenye bodi na watu wanaohusika na wizara za kilimo, na kusema kwamba korosho zilizo maghalani zinatafutiwa utaratibu.
Awali katibu msaidizi wa Idara ya vyuo na vyuo vikuu Taifa, Mwanaidi Kipingu alisema viongozi wanapaswa kuwaona vijana kuwa sehemu muhimu ndani ya chama hicho na kundi kubwa lenye hamasa katika chama badala ya kuwatumia kipindi cha uchaguzi pekee na kuwataka vijana kuwa msaada mkubwa wa kutoa elimu na kukipigania chama.
No comments:
Post a Comment