Polepole ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Juni Mosi, 2019 katika mahafali ya wanafunzi wanachama wa CCM wanaotarajiwa kumaliza elimu ya juu mkoani Mtwara.
Amesema wabunge wanaofanya hivyo wanapaswa kujipanga mapema, “Kama wewe ni CCM na unashiriki nongwa kwa jambo hili ambalo tumelifanya kwa uchungu mkubwa jipange mapema.”
“Jipange kwa sababu mimi na wenzangu kuanzia sekretarieti, kamati kuu na halmashauri kuu tupo kitu kimoja tumeweka mustakabali sawa kulinda utu na heshima ya wakulima.”
Ameongeza, “Hivi mtu akiwa anaonewa unamsaidia huwa unawaza baada ya kumsaidia inakuwaje au unahangaika kwanza kumsaidia. Unamsaidia kwanza na baadaye ndio mnazungumza. Nunua kwanza heshima ya watu isimame.”
Licha ya kutowataja majina lakini baadhi ya wabunge wa CCM wamekuwa wakikosoa utaratibu uliotumika kununua korosho.
Mei 20, 2019 sakata la korosho liliwasha moto kwa mara nyingine bungeni huku wabunge watatu wakiikalia kooni Serikali na kuitaka kutoa majibu yatakayowaridhisha juu ya mchakato mzima wa uuzwaji wa zao hilo nchini.
Wabunge hao walisema hayo wakati wakichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka wa Fedha 2019/2020.
Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye alianza kwa kuchangia hoja juu ya zao hilo akiwataka waliohusika kulihujumu wawajibike wenyewe na wasipofanya hivyo, atapeleka bungeni kusudio la kuwataja mmojammoja.
Nape alisema Rais John Magufuli alikuwa na nia njema lakini waliokwenda kutekeleza mchakato mzima wa ununuzi walikwenda kuua zao hilo. “Bahati mbaya zoezi lilikuwa na dhuluma, lilikuwa na rushwa lilikumbwa na ubabaishaji mwingi na uongo mwingi sana,” alisema waziri huyo wa zamani wa habari.
Alisema wapo wakulima ambao korosho zao zilichukuliwa, lakini hadi jana walikuwa hawajalipwa fedha zao na akaitaka Serikali kupeleka bungeni Sheria ya Korosho ili waipitie upya.
Katibu huyo wa zamani wa itikadi na uenezi wa CCM, pia alipendekeza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), akague na kupeleka ripoti bungeni jinsi kazi hiyo ilivyofanyika huku akidai iligubikwa na rushwa.
“Kama nilivyosema, Rais alikuwa na nia njema, lakini wengi wamemdanganya. Sasa ni vizuri wawajibike na mheshimiwa Spika ni vizuri tukawa specific. Si sahihi kuiingiza Serikali katika mambo yaliyofanyika ovyo,” alisisitiza Nape.
Nape hakuwa pekee yake katika mchango huo wa korosho ambao umekuwa ukijadiliwa bungeni karibu kila mara katika miezi ya karibuni.
John Mnyika (Chadema-Kibamba) na Joseph Selasini (Rombo-Chadema) nao siku hiyo walizungumzia kwa kina sakata la korosho.
No comments:
Post a Comment