Mbunge wa Viti Maalum (Chadema) Catherine Ruge amesema bajeti ya Serikali ya Tanzania ya mwaka 2019/2020 ya Sh33.1 trilioni ni bajeti ya vitu kwa sababu sehemu kubwa ya fedha za miradi ya maendeleo imepelekwa katika miradi ya umeme, ndege na reli.
Amesema hayo jana Alhamisi Juni 20, 2019 wakati akichangia mapendekezo ya bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2019/2020.
Ruge katika kudhibitisha ni bajeti ya vitu alinukuu Katiba na Ripoti ya Maendeleo ya Watu nchini ya mwaka 2017 ambayo ilitolewa na taasisi tatu ikiwa ni Shirika la Kimataifa la Maendeleo (UNDP), Wizara ya Fedha na Mipango na ESRF.
Amesema kipimo cha maendeleo ya watu kwa mujibu wa ripoti hizo katika maeneo makuu matatu ya maendeleo ya binadamu ambayo ni maisha bora kwa kuzingatia umri wa kuishi tangu kuzaliwa, ujuzi kwa kuashiria elimu, makadirio ya miaka ya masomo na pato la Taifa kwa mtu mmojammoja.
“Bajeti ya maendeleo ya wizara ya afya ni Sh500 bilioni sawa na asilimia nne ya bajeti yote ya maendeleo, ukienda kwenye maji ni Sh600 bilioni ambayo ni asilimia tano, ukienda kwenye elimu Sh863 bilioni sawa na asilimia saba,” amesema Ruge.
Amesema pato la Mtanzania Sh2.4 milioni kwa mwaka na kuhoji Sh200,000 kwa mwezi anayoipata inamwezesha kujikimu na kuondoka katika umasikini.
Amesema katika bajeti hiyo imeweka vipaumbele katika viwanda na kilimo.
Mbunge huyo amesema bajeti ya maendeleo ya wizara ya viwanda na biashara ni Sh51.5 bilioni sawa na asilimia 0.4 na bajeti kilimo ni Sh143.5 bilioni ambayo ni sawa asilimia 1.2.
“Sasa Watanzania wasikie na kupima kwa bajeti hii tunaweza kutoka hapa tulipo? Ukijumulisha bajeti yote ya viwanda, Kilimo, Elimu, Afya, Maji, Mifugo na Uvuvi unapata Sh2.1 trilioni sawa asilimia 17.3,”amesema.
Amesema ukienda katika maendeleo ya vitu hapo ndipo kuna mradi wa kufua umeme wa Rufiji, Reli ya Kisasa ya SGR.
Amesema bajeti ya maendeleo ya wizara ya ujenzi ni Sh1.2 trilioni, ukienda katika uchukuzi ni Sh3.5 trilioni ukienda katika nishati ni Sh2.1 trilioni na kwamba jumla ya bajeti hiyo ni Sh6.8 trilioni sawa na asilimia 58 ya bajeti yote ya maendeleo.
Amesema ni sawa kipaumbele ni kwenye kilimo na elimu lakini wameelekeza bajeti kubwa katika vitu vingine.
“Asilimia 20 ya bajeti yote inakwenda kwenye ujenzi wa SGR hivi tunawekeza ili kusafirisha bidhaa za Wachina kwenda Congo ama mazao ya Watanzania masikini,” amehoji.
Tunawekeza Stigler’s Gorge asilimia 12 ambayo inapeleka umeme viwandani hivi hivyo viwanda vina malighafi? Unaenda kuwekeza kwenye ndege Sh500 bilioni hivi hiyo atapanda nani wakati pato la Mtanzania ni Sh200,00?”.

No comments:
Post a Comment