Rais Hassan Rouhani amesema Iran haipingi mazungumzo na Washington, lakini haitokubali kushinikizwa. Mvutano umeongezeka sana katika wiki kadhaa zilizopita kati ya Marekani na Iran.
Rais wa Iran Hassan Rouhani amesema jana kwamba nchi yake iko tayari kwa mazungumzo na Marekani iwapo itaonyesha heshima na kufuata sheria za kimataifa. Lakini kiongozi huyo amesema Iran haitokubali kushinikizwa na Marekani kwenda kwenye meza ya mazungumzo.
"Tuko tayari kwa mazungumzo iwapo upande mwingine utakaa kwa heshima katika meza ya mazungumzo na kufuata kanuni za kimataifa, lakini sio kutoa amri ya majadiliano," Rouhani amesema kulingana na Fars.
Mivutano kati ya Iran na Marekani imeongezeka kwa kasi kubwa katika miezi ya hivi karibuni. Marekani inasema Iran ni kitisho kwake na washirika wake bila ya kutoa ufafanuzi zaidi.
Mara kwa mara Rouhani amekuwa akikataa kukaa katika meza ya mazungumzo mpaka pale Marekani itakapoviondoa vikwazo vya kibiashara ilivyoiwekea Iran, pamoja na kurudi katika makubaliano ya nyuklia yaliyosainiwa mwaka 2015 kati ya Marekani, Iran na mataifa mengine yenye nguvu duniani.
Mvutano kati ya nchi hizo mbili ulianza baada ya Marekani kujitoa katika makubaliano hayo mwaka jana na kuiwekea vikwazo zaidi Iran.
No comments:
Post a Comment