Yanga imeendelea kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi baada ya kuichapa Tanzania Prisons mabao 2-1 katika mchezo uliopigwa uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam
Yanga iliyokuwa bora katika mchezo wa leo, ilifunga mabao yake kupitia kwa Wacongomani Papi Tshishimbi na Heritier Makambo wakati bao la kufutia machozi kwa upande wa Prisons lilifungwa na Ismail Kada
Tshishimbi ndiye aliyeanza kuifungia Yanga bao la kuongoza kwenye dakika ya 23 akimalizia mpira wa adhabu uliochongwa na Ibrahim Ajib
Hilo lilikuwa bao la 16 kutengenezwa na Ajib msimu huu
Dakika tisa baadae Kada aliisawazishia Prisons akiujaza mpira wavuni baada ya walinzi wa Yanga kuzembea kuondoa mpira wa kona
Makambo aliihakikishia Yanga ushindi kwenye dakika ya 66 akiunganisha kwa kichwa krosi ya Paulo Godfrey 'Boxer'
Ushindi huo umeifanya Yanga kuwa timu ya kwanza kufikisha alama 80 msimu huu na kuendelea kujikitia kileleni mwa msimamo wa ligi kwa tofauti ya alama nane dhidi ya Simba inayoshika nafasi ya pili ikiwa na alama 72
Baada ya ushindi huo, Yanga itaelekea mkoani Iringa tayari kwa mchezo wa nusu fainali kombe la FA (ASFC) dhidi ya Lipuli, mchezo ukitarajiwa kupigwa Jumapili, May 05
No comments:
Post a Comment