Yanga inaendelea na mchakato wa kuboresha kikosi chake ambapo nyota kadhaa wameendelea kupishana Makao Makuu ya klabu hiyo kumwaga wino
Uongozi wa Yanga bado haujaweka hadharani orodha ya wachezaji ambao tayari imeshawasajili
Lakini sababu kubwa ni moja, wapo ambao mikataba yao haijamalizika kwenye klabu wanazotoka, kuwatangaza sasa kutaiingiza timu hiyo matatani
Lakini ukweli ni kwamba michakato inaendelea na taarifa nyingi zinazotolewa kuhusu usajili wa Yanga ni sahihi, kinachosubiriwa ni uthibitisho tu pale kila kitu kitakapokuwa kimekamilika
Mpaka jana jioni inaelezwa Yanga tayari ilikuwa imemalizana na wachezaji tisa, wengine wakiwa tayari wamesaini, baadhi walikuwa wako katika hatua za mwisho za mchakato
Wachezaji ambao wamemalizana na uongozi wa timu hiyo ni pamoja na walinzi Lamine Moro, Mohammed Ali Camara, Ali Sonso na Ali Ali.
Viungo Isa Birigimana, Patrick Sibomana na Abdulaziz Makame
Mlinda lango Farouq Shikalo amesaini mkataba wake akiwa kwao nchini Kenya wakati mshambuliaji kutoka ZESCO Maybin Kelengo alitarajiwa kusaini mkataba jana
Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera alisema atasajili wachezaji nane wa kigeni na wanne wazawa kukamilisha idadi ya wachezaji 12
Mpaka sasa wachezaji wa kigeni wako sita na wazawa watatu, hivyo bado wageni wawili na mzawa mmoja
Msimu uliomalizika Yanga ilikuwa na wachezaji watano wa kigeni, Klaus Kindoki, Papi Tshishimbi, Thabani Kamusoko, Amissi Tambwe na Heritier Makambo
Tshishimbi ameongeza mkataba wa kuendelea kuitumikia Yanga wakati Makambo ameondoka Yanga kujiunga na Horoya AC
Kamusoko yuko Zimbabwe akitimiza majukumu ya timu ya Taifa, tayari alishawaaga wachezaji wenzake
Kindoki na Tambwe huenda wakawania nafasi moja ya mchezaji wa kigeni itakayokuwa imebaki kama Zahera atafanikiwa kusajili wapya nane wa kigeni
Kindoki bado ana mkataba wa mwaka mmoja na Yanga, hivyo ni Tambwe ambaye yuko kwenye hatihati ya kuachwa kwa kuwa mkataba wake umemalizika
Hata hivyo inaelezwa viongozi wa Yanga wamemwambia asubiri, mazungumzo ya mkataba mpya yanaweza kufanyika
No comments:
Post a Comment