Waendesha Mashitaka wa Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamefuta uchunguzi wa shitaka la jinai dhidi ya Moise Katumbi, mwanasiasa wa upinzani ambaye kwa sasa yuko uhamishoni.
Moise Katumbi alikuwa anakabiliwa na mashtaka ya kuajiri askari mamluki wa kigeni wakiwemo askari kadhaa wa Kimarekani waliostaafu kwa lengo la kuangusha utawala uliopita wa Joseph Kabila.
Timothee Mukuntu, Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Kijeshi wa DRC alitoa rasmi tangazo hilo jana Jumanne na kufafanua kuwa, "Kwa kuzingatia kuwa rais wa Jamhuri ametoa kipaumbele kwa suala la kupunguza taharuki za kisiasa, tumeona kuwa ni vyema tufutilie mbali uchunguzi huo."
Ingawaje waraka kuhusu tangazo hilo ulitiwa saini tarehe Mosi mwezi Machi, lakini uliwekwa hadharani kwa umma jana Jumanne. Wakili wa Katumbi amesema huu ni wakati mwafaka kwa mteja wake kurejea nyumbani. Hata hivyo Katumbi mwenyewe hajazungumza chochote kuhusu uamuzi huo.
Septemba mwaka jana, Ofisi ya Mashtaka ya Umma nchini humo ilimzuia Moise Katumbi kuwania urais na kutishia kuwa angelikamatwa iwapo angelitia mguu wake nchini DRC, akikabiliwa na tuhuma za kuhatarisha usalama wa taifa. Felix Tshisekedi alitangazwa mshindi wa uchaguzi huo wa urais wa Disemba mwaka jana 2018.
Meya huyo wa zamani wa Katanga mwenye umri wa miaka 54, alikimbilia uhamishoni mwezi Mei mwaka 2016 baada ya kuhitilafiana kisiasa na rais mstaafu Joseph Kabila.
No comments:
Post a Comment