Serikali imekabidhiwa mali zilizotaifishwa na mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Mwanza yakiwemo madini aina ya dhahabu zaidi ya kilo 325 yenye thamani ya shilingi bilioni 27 ambayo yalikuwa yanatororshwa na wafanyabiashara wa madini walioshirikiana na askari.
Januari 5 mwaka huu madini hayo yalikuwa yanatoroshwa kutoka Mwanza kuelekea Geita bila kuwa na kibali huku ikidaiwa kuwepo kwa mazingira ya rushwa wakati wa utoroshwaji wa madini hayo hali iliyopelekea watu 12 wakiwemo askari polisi 8 kukamatwa na kufikishwa mahakamani.
Januari 28, 2019 mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Mwanza, ilianza kusikiliza kesi namba 1 ya uhujumu uchumi iliyowahusisha washtakiwa 12 wakiwemo wafanyabiasha 4 na askari polisi 8 ambapo machi 27 mahakama hiyo ilitaifisha madini, fedha pamoja na mali zilizokuwa zinatoroshwa kufuatia wafanyabiashara hao kukiri makosa huku askari nane wakikana makosa yao ambapo hadi sasa kesi dhidi ya askari hao bado inaendelea.
Akikabidhi kwa serikali madini, fedha na mali zilizokuwa zinatoroshwa mkurugenzi wa mashtaka nchini DPP Biswalo Mganga, akatumia fursa hiyo kuvishukuru vyombo ya ulinzi na usalama kwa namna vilivyotoa ushirikiano katika kufanikisha kukamatwa kwa vitu hivyo.
Akipokea fedha, mali pamoja na dhahabu naibu katibu mkuu wizara ya fedha na mipango Khatibu Kazungu, amesema fedha hizo zimeshafika na zitafanya shughuli mbalimbali za kijamii.
Dotto Biteko ni waziri wa madini akawaasa wafanyabiashara wa madini kuacha kujihusisha na tabia ya utoroshaji wa madini na badala yake wafate sheria za nchi ikiwemo na kupenda kulipa kodi.
No comments:
Post a Comment