Baadhi ya Wanawake wa Kijiji cha Ngereyani, Kata ya Tinga Tinga, Tarafa ya Enduiment wilayani Longido, wamelaani kitendo cha wanaume kuwaachia majukumu ya kifamilia kinyume na taratibu.
Akizungumza Maria Saningo mkazi wa kijiji hicho, alidai jamii ya kifugaji imekuwa ikiwatelekeza wanawake na majukumu ya kifamilia hali ambayo hulazimika kufanya biashara ya uuzaji wa mkaa ili waweze kuendesha familia zao.
Alisema wanawake wengi wa kifugaji wanatamani kuwa wajasiriamali, lakini kutokana na waume zao kuwanyima kufanya biashara wameishia kwenye uharibifu wa mazingira kwa kukata miti na kuchoma mkaa.
Alieleza wanawake wakipatiwa elimu na kuwezeshwa mikopo midogo midogo, wataweza kuondokana na adha ya uharibifu wa mazingira, kwa kuwa wanafanya hivyo kutokana na hali ngumu ya maisha wanayoishi.
"Hali ni ngumu na tumeachiwa majukumu, tunalazimika kuchoma mkaa, tulee familia zetu, naomba serikali itizame hili, watoto wanahitaji elimu, afya, chakula na mavazi twende wapi kama wanaume wanakwepa majukumu yao," alihoji Maria.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Ken ole Moloimet, alikiri kuwapo kwa tabia ya baadhi ya wanaume kuwaachia wanawake majukumu, nakuomba mashirika yenye uwezo wakuwawezesha wanawake hawa katika makundi ya ujasiriamali kujitokeza na kuwaunga mkono
"Ni kweli sipingi jamii ya Kimaasai wanawake ndiyo wanaowajibika kwa asilimia kubwa kulea na kutunza familia zao," alisema Moloimet.
Lakini pia niwatake wawe wavumilivu katika kipindi hiki kigumu kwa sababu uharibifu wa mazingira unasababisha ukame lakini pia tutakosa watalii kuja kutembelea hifadhi ya Enduiment kwa sababu ya mazingira si rafiki.
No comments:
Post a Comment