Kwanza, wana kikosi kipana chenye wachezaji wa daraja la juu ukilinganisha na wapinzani wao, Yanga na Azam huku jeuri ya uwekezaji wa MO Dewji ukinogesha mzuka wa kupata matokeo mazuri uwanjani.
Lakini, jambo ambalo lilikuwa likiwapa presha mabosi wa Wekundu hao wa Msimbazi ni kuhusiana na mastaa wake wakubwa, ambao mikataba yao ndiyo inaelekea ukingoni mwishoni mwa msimu huu.
Sasa Bodi ya Simba chini ya uenyekiti wa MO ikakuna kichwa na kufanya mambo kisomi kwa kuwaweka chini mastaa wake ili kuhakikisha msimu ujao wanavaa tena jezi zake na kuendeleza ubabe kwenye michuano ya kimataifa na kufika mbali zaidi.
Wakati mastaa hao wakianza kuwekwa wazi ili kupewa mikataba mipya, suala la uhakika wa kubaki ama kuondoka kwa Kocha Mbelgiji Patrick Aussems nalo likapewa fursa na ikakubaliwa japo siyo rasmi kwamba, atapewa mkataba mpya.
Majembe hayo ambayo Simba imeanza kuwaweka sawa ni nahodha wake John Bocco, Jonas Mkude, Aishi Manula, Erasto Nyoni na Shomary Kapombe, ambaye bado ni majeruhi ingawa ameshaanza mazoezi yake binafsi.
Majembe haya yote yalikuwa kwenye msimu wa mwisho kukipiga na Simba kwani, mikataba yao ndiyo inafikia ukingoni na mabosi wa Simba wamefichua kwamba, kwa kuanzia wazawa ndiyo watapewa kipaumbele.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori alisema wachezaji hao wanamaliza mikataba yao na wamekuwa tegemeo kwenye kikosi cha Msimbazi kwa sasa.
Alisema kwa sasa wako kwenye hatua za mwisho za kuanzisha mazungumzo ili kuwapa mikataba mipya wachezaji hao na kwamba, hakuna ambaye ataondoka klabuni hapo kwa sasa.
Magori aliongeza kuwa baada ya kumalizana na majembe hayo matano, awamu itakayofuata itakuwa ni kwa ajili ya mastaa wa kigeni ambao mikataba inamalizika pamoja na wapya ambao, wataongezwa kikosini hapo.
“Hatujaanza kuzungumza na mchezaji yeyote mpya, ambaye tutamtaka aje kuongeza nguvu kikosini kwetu kwa ajili ya msimu ujao. Tuko kwenye mchakato wa kukamilisha kazi ya kuwasainisha mikataba mipya hawa kwanza kisha tutaangalia wachezaji wengine kulingana na upungufu wa timu. “Msimu ujao tutatoka kivingine kabisa na ndiyo sababu tunataka kubakiza wachezaji muhimu ambao mikataba yao inaelekea mwishoni. Tumejipanga kuendesha mambo yetu kisasa zaidi,” alisema.
No comments:
Post a Comment