Ofisi ya Afisa Madini Mkazi, Mkoa wa Kimadini wa Kahama inatarajia kuanzisha soko la madini mapema ikiwa ni moja ya mikakati ya Serikali kupitia Wizara ya Madini katika kudhibiti utoroshwaji wa madini.
Hatua hiyo imekuja kufuatia ziara ya Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo aliyoifanya mapema leo tarehe 30 Machi, 2019 katika Wilaya ya Kahama lengo likiwa ni kukagua shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa madini ya dhahabu, kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji wa madini.
Katika ziara hiyo, Naibu Waziri Nyongo aliambatana na Kamishna Msaidizi- Uendelezaji Migodi na Madini wa Wizara ya Madini, Ali Said Ali wataalam kutoka Tume ya Madini pamoja na wawakilishi wa vyombo vya ulinzi na usalama.
Mara baada ya kufanya ziara katika baadhi ya mitambo ya kuchenjua dhahabu, Nyongo alifanya kikao na wamiliki wa mitambo hiyo na kusikiliza kero mbalimbali pamoja na kuzitatua.
Mara baada ya kusikiliza kero husika ikiwa ni pamoja na ya kutokuwepo kwa soko la madini katika Wilaya ya Kahama, Naibu Waziri Nyongo alimwelekeza Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kimadini wa Kahama, Adrea Fabian kuhakikisha sehemu ya ofisi yake inatumika kama soko la madini ya dhahabu ambapo wauzaji na wanunuzi watakuwa wanafanya biashara huku serikali ikipata mapato yake, kauli ambayo ilipokelewa kwa shangwe na wafanyabiashara wa madini ya dhahabu.
Aidha aliendelea kusema kuwa kutokuwepo kwa soko la madini katika Wilaya ya Kahama, kunachochea utoroshwaji wa madini ya dhahabu kwakuwa inakuwa vigumu kwa wauzaji wa madini hayo kusafiri umbali mrefu hadi Geita kwa ajili ya kwenda kuuza madini hayo.
No comments:
Post a Comment