Mkuu wa Mkoa wa Iringa Ally Hapi amewaagiza wafanyabiashara wanaokopesha fedha kwa watu mbalimbali mitaani mkoani Iringa, kujisalimisha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili wakadiriwe kodi na walipe kama ilivyo kwa biashara nyingine.
"Kama wanafanya biashara hiyo bila ya kuwa na leseni ya biashara hiyo naagiza vyombo vya dola na mamlaka zingine zinazohusika ziwasake na kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria," alisema mjini Mafinga katika kampeni yake ya Nawafuata Mlipo.
Kampeni hiyo iliyoanza kutekelezwa wiki iliyopita katika halmashauri ya Manispaa ya Iringa na itakayofanyika katika halmashauri zote za mkoa wa Iringa, inalenga kupokea na kusaidia kuipatia ufumbuzi migogoro ya ardhi, nyumba, mipaka na mashamba mkoani humo.
Akizungumza na wananchi wa Mji wa Mafinga waliojitokeza kuwasilisha kero hizo, Hapi alisema "Nimetoa uamuzi huo baada ya kubaini kuwepo na wafanyabishara hao mjini Iringa, wanaokopesha fedha watu mbalimbali kwa riba kubwa na wanaposhindwa kufanya marejesho, kutaifishiwa mali zao zikiwemo nyumba."
Akitoa mfano alisema yupo mama mmoja mjane (hakumtaja jina) aliyewasilisha kero yake katika mikutano yake mjini Iringa ambaye alikopa Sh 600,000 kwa dhamana ya hati ya nyumba yake kwa mmoja wa wafanyabishara hao ambazo zilizaa hadi Sh milioni 10 katika kipindi kisichozidi miaka miwili.
No comments:
Post a Comment