Na Thabit Madai Zanzibar.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Abdullah Juma Mabodi aliwataka viongozi wa majimbo yote kujitokeza katika majimbo yao kufanya mikutano na wananchi ili kujua shida zao na kuzitekeleza
Hayo ameyasema huko katika Uwanja wa Mzalendo jimbo la Magomeni wakati alipokuwa akizungumza na wanachama wa jimbo hilo kwenye uzinduzi wa gari aina ya basi lililotolewa na Mbunge.
Amesema viongozi wa majimbo wakionana na wanachama ndipo watapopata kujua kero zao na kuweza kuwatatulia kuwafahamisha kila walichowafanyia ikiwa ni moja ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi kama anavyohimiza Mh Rais wa Zanzibar.
“Jishusheni katika majimbo yenu mjielezee mlichowafanyia wanachama wenu ili wafarijike na pia muweze kusikiliza shida zao kwa lengo la kuwatimizia pamoja na kutimiza ahadi zenu kwa kuwafanyia mikutano”,alisema Mabodi.
Hivyo amewaomba wanachama wa jimbo hilo kulitumia vizuri gari hilo kwa kulitunza ili liweze kutumika kwa muda mwingi katika shughuli mbali mbali zote za kijamii ambalo hilo ni gari la pili katika kutolewa jimboni hapo.
Mabodi amewapa onyo wale wote wanaotaka kuleta uvunjaji wa amani na kuwataka kushughulikia kazi zao za kujiletea maendeleo na kuachana mara moja na mambo yasiyofaa kwani hawatafumbiwa macho kwa kila anaetaka kuichezea amani nchini.
Vile vile alisema Chama cha Mapinduzi hakina historia ya kusema mafanikio halafu isitekekleze , inatekeleza kwa vitendo na wananchi wote wanaona hii ni miongoni mwa utekelezaji wa ilani ya chama.
Nae Mbunge wa Jimbo hilo Mh Jammal Kassim amewataka vijana kuzitumia fursa alizozitoa ikiwemo kutoa mafunzo ya ujasiriamali wa utengenezaji wa sabuni., batiki ili waweze kukabiliana na mazingira magumu kwa kuweza kujiajiri wenyewe.
Pia amewataka wale waliokosa fursa ya kuendelea mbele katika masomo yao kuungana na vijana wenzao ili waweze kupata elimu mbali mbali zinazotolewa katika jimbo hilo na kuacha kukaa kwenye magenge yasiofaa.

No comments:
Post a Comment