Mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Muhuwesi, Tariq Mohamed (16), amefariki dunia katika tukio la kutatanisha na kuporwa baiskeli na karanga ambazo alikwenda kuzichukua shambani baada ya kutumwa na wazazi wake.
Tukio hilo lilitokea juzi baada ya mwanafunzi huyo kutorejea nyumbani kutoka shambani kufuata karanga ambazo zilipangwa kwa matumizi ya kuungia mboga.
Imeelezwa kuwa watu waliofanya unyama huo, kabla ya kumuua, walimfunga kitambaa usoni na kamba mikono yake kwa nyuma.
Baba mzazi wa kijana huyo, Issa Mohamed, alisema mtoto huyo alitumwa na mama yake mzazi, Sofia Said, kwenda kufuata karanga hizo shambani baada ya kurudi kutoka shuleni.
Inadaiwa kuwa siku hiyo kulikuwa na mitihani ya majaribio kwa wanafunzi wa darasa la saba, hivyo wanafunzi wengine hawakutakiwa kuwapo shuleni ili kuwezesha kuleta utulivu.
Alisema baada ya kupokea taarifa za kutorejea kwa kijana wake, aliambatana na watu watatu kwa ajili ya kwenda kumtafuta bila mafanikio na kwamba baada ya hapo, alitoa taarifa kwa uongozi wa serikali ya kijiji na kata na baadaye kituo cha polisi kwa ajili ya msaada zaidi.
Mohamed alisema siku ya pili, wananchi wakisaidiana na viongozi wa serikali ya kijiji na kata, walifanya msako katika eneo la njia ya kuelekea mashamba yaliyoko katika eneo la Chasa na kuukuta mwili wa kijana huyo ukiwa umetelekeza katika vichaka.
Mganga aliyeufanyia uchunguzi mwili wa Tariq, Dk. Alfred Mabena, alisema kifo hicho kilisababishwa na tukio la kunyongwa na kuvunjwa mifupa ya shingo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Simon Marwa, amedhibitisha kuwapo kwa tukio hilo na kwamba polisi wanamshikilia Noel Nasoro kwa ajili ya uchunguzi.
No comments:
Post a Comment