Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema amechambua uamuzi wa aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa kurejea CCM.
Lema amedai kuwa uamuzi wa Lowassa unadhihirisha kuwa ameweka mbele maslahi yake binafsi kuliko mabadiliko aliyokuwa anayahubiri alipoingia Chadema.
Alidai kuwa Lowassa alifikia uamuzi huo ili kulinusuru shamba lake linaloshikiliwa Mkoani Tanga, shamba lake la mifugo linaloshikiliwa Dodoma pamoja na kumnusuru mkwewe Sioi Sumari na kifungo dhidi ya kesi inayomkabili. Sumari anatuhumiwa kwa kula njama ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, kughushi pamoja na utakatishaji wa fedha.
“Mtu huyu alitaka kuwa Rais, hali ya kisiasa ilivyo sasa watu wapo magerezani, wanapata misukosuko ya kibiashara, hawana cha kuipa CCM ili wapate ahueni, lakini kwa sababu yeye anacho cha kuwapa CCM ilia pate amani. Hajaona gharama ya kufanya hivyo,” Mwananchi wanamkariri Lema.
“Chadema imepata baraka kuondokewa na mtu kama huyu. Alikuja kwa ajili ya kutaka urais na sio mabadiliko aliyokuwa akiyanadi. Nchi inataka demokrasia, katiba mpya, sheria mpya na inakabiliwa na ubanaji wa vyombo vya habari… mwanasiasa makini hawezi kuungana na CCM,” aliongeza.
Hata hivyo, mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari alikiri kuwa kuondoka kwa Lowassa kunahuzunisha.
“Lowassa ni mtu mzima anajua anachokifanya. Lakini wakati anajiunga Chadema ilikuwa imara na huku Kaskazini ilikuwa ya Upinzani. Hatuumii ila inahuzunisha,” Mwananchi wanamkariri Nassari.
Aidha, kuondoka kwa Lowassa kumepokewa kwa mitazamo tofauti na wapinzani, ambapo Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa amesema chama hicho kimeamua kutozungumzia suala hilo na kuendelea kujenga chama chao.
Lowassa alijiunga na Chadema mwaka 2015 baada ya jina lake kuondolewa kwenye kinyang’anyiro cha watu waliokuwa wakiwania nafasi ya kugombea urais kwa tiketi ya CCM. Aligombea urais na kuleta ushindani mkubwa dhidi ya Dkt. John Magufuli wa CCM.
Juzi alipokewa na Dkt. Magufuli, Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Lowassa alieleza kwa ufupi kuwa amerejea nyumbani. Alipokewa katika Ofisi ndogo za Makao Makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment