Serikali ya Mapinduzi Zanzibar SMZ kupitia Wizara ya Afya, Kitengo cha kumaliza Malaria Zanzibar leo rasmi wameanza upigaji wa Dawa Majumbani ili kutokomeza Malaria.
Akizindua zoezi hilo Mkuu wa Wilaya ya Kati Mashavu Said Sukwa amewataka Wananchi kuonesha ushirikiano wakati wa zoezi hilo ili kuutokomeza kabisa Ugonjwa huo.
Mkuu huyo wa Wilaya amewataka Wananchi wa shehia ya Miwani, Wilaya ya Kati waliokusanyika katika Uwanja wa Mpira wakati wa uzinduzi huo kuhakikisha wanawafikishia Taarifa wengine ambao hawakuwepo ili kuwarahisishia Wapigaji dawa kufanya kazi yao kwa ufanisi.
Amesema Serikali inafanya juhudi kubwa na gharama nyingi ili kuona Wananchi wake wanaishi kwa usalama wa Afya zao hivyo Wananchi hao wanapaswa kuunga Mkono Serikali yao.
“Serikali inatumia gharama kubwa katika kuliondosha tatizo hili hivyo Wananchi toeni ushirikiano kwa wapiga dawa ili muweze kuondosha kabisa Ugonjwa huu ambao ni hatari sana”, alisema Sukwa.
Amefahamisha kuwa Malaria ni Ugonjwa hatari sana unaopelekea athari kubwa katika jamii ikiwemo kuweza kusababisha ulemavu wa Viungo pale unapopanda Kichwani.
Aliwapongeza Wananachi wa Wilaya yake kwa kazi nzuri za kujitolea na mashirikiano wanayoyatoa katika shughuli za kitaifa na kijamii hivyo anaamini zoezi hilo litaenda vizuri
Akielezea kuhusu Jiografia ya Wilaya ya Kati Mkuu huyo amesema Wilaya hiyo ina jumla ya Shehia 31 na Nyumba 513 ambazo zinatarajiwa kupigwa dawa.

No comments:
Post a Comment