Muungano wa wabunge wa wanawake kutoka jamii za wafugaji Kenya wamependekeza sheria kuhusu dhuluma za kimapenzi ifanyiwe marekebisho ili wabakaji waadhibiwe kwa kukatwa uume.
Katibu mkuu wa muungano huo Rehema Jaldesa alisema amewasilisha mswada kielelezo kwa Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi akipendekeza mabadiliko kwa kipengele cha 43 cha sheria hiyo.
“Nimewasilisha pendekezo langu kwa Spika wa Bunge kwa njia ya muswada wa marekebisho nikitaka adhabu ya kifungo cha miaka 10 kwa watakaopatikana na hatia ya kubaka wasichana wadogo ibadilishwe na badala yake nyeti zao zikatwe,” alisema.
Jaldesa ambaye ni mwakilishi mwanamke wa Isiolo alisema adhabu hiyo ndio njia mwafaka ya kumaliza unyama huo ambao hufanyiwa watoto wa kike hasa katika jamii za wafugaji.
“Kuna haja gani kwa mwanaume ambaye amembaka mtoto wa kike kufungwa jela kwa miaka 10 baada ya kuharibu kabisa maisha ya mtoto huyo?” Akauliza.
Jaldesa alitoa mfano wa hali ilivyo nchini Saudi Arabia ambapo wizi umemalizwa kabisa kutokana na adhabu ya wezi kuwakata mikono wanapopatikana na hatia.
“Hata hivyo, nia yangu si kuona wanaume wasio na hatia wakikandamizwa bali wale ambao wana tabia mbaya ya kuwabaka hata watoto wao wenyewe,” alisema.
Mbunge huyo alisema wakati wa uzinduzi rasmi wa muungano huo ambao ni kitengo cha Kundi la Wabunge kutoka Jamii za Wafugaji (PPG).
Miongoni mwa waliohudhuria shughuli hiyo ni wabunge Soipan Tuya (mbunge mwakilishi, Narok), Sarah Korere (Laikipia Kaskazini), Ruweidha Obbo (Mbunge Mwakilishi, Lamu), Janet Teyia (Kajiado), Abushiro Halake (Seneta Maalum) na Naomi Jillo (Seneta Maalum)
Jillo ambaye ni mwenyekiti wa muungano huo alisema lengo lao ni kupambana na maovu ambayo wanafanyiwa watoto wa kike na wanawake katika jamii zao.
“Nia yetu ni kupambana na maovu kama vile ubakaji wa wanawake na watoto wa kike, ukeketaji wa wasichana, ndoa za mapema na kutengwa kwa mwanamke katika masuala ya umiliki wa ardhi na uwakilishi wa kisiasa,” alisema.
Jillo alisema njia mwafaka ya kukomesha maovu hayo ni kuendeleza uhamasisho ili wanawake wengi waweze kupigania nafasi za uongozi kupitia chaguzi.
“Ni fahari yetu kwamba kufikia sasa idadi ya wabunge na maseneta wanawake ni 28 waliochaguliwa au kuteuliwa katika uchaguzi mkuu, mfano, kwa mara ya kwanza mwanamke amechaguliwa kuwa seneta katika eneo la Kaskazini mwa Kenya’’alisema.
“Katika uchaguzi wa 2022 tuna matumaini wanawake wengi watachaguliwa kuwa magavana, meseneta na wabunge,” Jillo alisema.

No comments:
Post a Comment