Simba ilitua jana nchini Misri tayari kuwakabili mabingwa soka nchini humo Al Ahly katika mchezo wa ligi ya mabingwa, raundi ya tatu kundi D
Wakati akifanya mahojiano na kituo cha runinga cha Sada El- Balad, Aussems amesema wamejindaa kuikabili Al Ahly wakitambua ni timu yenye mafanikio na bora zaidi katika kipindi cha miaka 10 iliyopita
Akizungumza na mwandishi wa runinga hiyo, Aussems alisema timu yake haina matumaini makubwa ya kuibuka na ushindi kwenye mchezo huo wa ugenini lakini wanaamini watafanya vizuri zaidi katika michezo ya nyumbani
"Ni mechi muhimu mno. Tunajua tunakutana na timu imara zaidi Afrika kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita. Tunapaswa kufanya kazi ya ziada ili kuweza kuondoka na chochote hapa"
"Niwe mkweli, sikutarajia na sidhani kama tunaweza kupata pointi ugenini dhidi ya AS Vita na Al Ahly. Mkazo wetu ni kukusanya pointi nyingi nyumbani kadiri tunavyoweza"
"Huwa sipendelei ndoto, hatuwezi kupata pointi hapa dhidi ya Al Ahly kwa kuwa watapewa penati, mchezaji wetu anaweza kuonyeshwa kadi nyekundu wakati wowote na wanaweza wakapewa hata bao la kuotea ili mradi tu washinde," alisema
Mwamuzi wa mchezo huo ni Maguette N'Diaye ambaye anasifika kwa kuzibeba timu za waarabu katika michezo yote aliyochezesha timu hizo zikiwa dimbani
Takwimu zinaonyesha hakuna mchezo ambao mwenyeji alikuwa timu ya kiarabu na ikapoteza wakati mwamuzi huyo akiwa katikati ya dimba
Katika mchezo wa kwanza Al Ahly ilipokuwa nyumbani dhidi ya Vita Club, alichokisema kocha Patrick Aussems ndicho kilichotokea kwani beki wa Vita Club Kalondji alionyeshwa kadi nyekundu yenye utata kwenye dakika ya 35, kadi iliyobana Vita ambao walilazimika kucheza zaidi ya dakika 55 wakiwa wachezaji 10 uwanja na kuwarahisishia Al Ahly kuibuka na ushindi wa mabao 2-0
Licha ya mazingira hayo, wachezaji wa Simba wameahidi kupambana mpaka dakika ya mwisho kuhakikisha wanaondoka japo na alama moja kama watashindwa kuibuka na ushindi ambao kama ukipatikana, utakuwa wa kihistoria
No comments:
Post a Comment