Washambuliaji Juma Balinya, Sadney Urikhob na Patrick Sibomana kwa mara nyingine, watakiongoza kikosi cha Yanga kwenye mchezo wa kwanza wa ligi ya mabingwa dhidi ya ZESCO United utakaopigwa leo Jumamosi kwenye uwanja wa Taifa
Balinya na Sadney walikuwa jijini Mwanza kwenye kambi ya maandalizi kuelekea mchezo huo wakati Sibomana alirejea kwao Rwanda kutimiza majukumu ya timu ya Taifa
Hata hivyo Sibomana 'PS' amerudi akiwa 'fit' na hivyo kuongeza matumaini kuelekea mchezo huo
Moja ya changamoto zilizoikabili Yanga kwenye michezo ya hivi karibuni ni uhaba wa mabao
Hata hivyo kocha Mwinyi Zahera amesema changamoto hiyo imefanyiwa kazi
Katika michezo miwili ya kirafiki ambayo Yanga ilicheza jijini Mwanza, walifunga mabao manne na kuruhusu bao moja
Licha ya David Molinga ambaye alifunga mabao matatu kwenye ziara hiyo kukosekana, Zahera amesema ana imani na washambuliaji hao watatu
"Balinya ameonyesha mabadiliko, nlizungumza nae na kumjenga kisaikolojia, nadhani sasa atafunga mabao mengi" alisema Zahera
"Huyu ni mshambuliaji aliyekuwa mfungaji bora ligi kuu ya Uganda akifunga mabao 21 msimu uliopita, sina wasiwasi na uwezo wake"
"Sadney pia alikuwa na matatizo ya kukosa kujiamini. Kambi ya Mwanza imetusaidia kufanyia kazi mapungufu yote"
"Mashabiki waje kwa wingi uwanjani, tumejiandaa kushinda mchezo huo"

No comments:
Post a Comment