Na Omary Mngindo, Bwawani
NG'OMBE 12 wanaomilikiwa na Seif Lukake mkazi wa Kijiji cha Visakazi Kata ya Ubena Chalinze, Bagamoyo Pwani, wameshambuliwa kwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili, ikiwemo watatu kuvunjwa miguu.
Tukio hilo lililotokea usiku wa kuamkia Jumanne ya Sept 10 kijijini hapo, inadaiwa kwamba mifugo hiyo iliingizwa kwenye shamba la mkazi aliyetajwa kwa jina moja tu la Daud, mtoto wa mzee Maarufu kijijini hapo aitwaye Mzee Selemani.
Wakizungumza na Waandishi wa habari eneo la tukio, Surian Sosopi Mwenyekiti wa Chama Cha Wafugaji (CCWT) Kata ya Ubena, alisema kuwa alipewa taarifa ya kuwepo kwa tukio hilo, lililofanyika mbele ya Seif ambaye ndio mwenye ng'ombe hao.
"Hili tukio nilijulishwa jana usiku, kutokana na muda huo kutokuwa rafiki sikuweza kuja, leo asubuhi nimefika hapa na kama nilivyowaonesha, ng'ombe wapo 12 kati ya hao watatu wamevunjwa kabisa miguu," alisema Sosopi.
Mtendaji wa Kijiji hicho Ramadhani Tiku alisema kuwa alipigiwa simu usiku kujulishwa tukio hilo, akawajulisha askari Mgambo ambao walifika eneo husika ambapo waliweka ulinzi wa kuwadhibiti ng'ombe hao mpaka asubuhi.
"Daud ndio mwenye shamba akinijuza kuwa kuna kundi la ng'ombe limeingia shambani kwake, niliwapigia askari wa Mgambo, walifika hapa kwa ajili ya kulinda ng'ombe hawa ambao hawawezi hata kusimama," alisema Tiku.
Aliongeza kuwa wakati akitoa maelezo kwa Mwenyekiti wa Kamati ya usuruhishi ya kufanyika kwa tathimi, mtuhumiwa akachukua panga na kuanza kuwakatakata ng'ombe mbele ya mmiliki huyo aliyekuwa tayari kufanya mazungumzo na kulipa gharama husika.
Sada Mdeka Mjumbe Kamati ya usuruhishi kati ya wafugaji na wakulima alisema kuwa, Daud amekuwa na tabia ya ubabe, na kwamba hata panapofanyika mazungu ya kusuruhisha migongano, yeye hufika na kuwashawishi wakulima wawafikuze wafugaji.
Akizungumzia tukio hilo, Seif mmiliki wa ng'ombe hao aliwashukuru wafugaji wenzake waliomsikiliza, baada ya kuwaomba wasifanye fujo kwani hali ingekuwa mbaya zaidi.



No comments:
Post a Comment