Dk Msolla alichimba mkwara huo jana Jumapili jijini Arusha wakati akijibu maswali ya wanachama wa klabu hiyo juu ya jezi mpya zilizozinduliwa na kutangazwa bei yao ikiwa kati ya Sh 30,000-35,000.
Alisema jezi zinazoonekana mitaani kwa sasa ni halisi ambazo za mashabiki ni Sh 30,000 na zile zinazotumiwa na wachezaji ni Sh 35,000 na kampuni iliyopewa tenda ya kusambaza ni GSM, lakini kama watashtukia jezi feki kokote walipo watoe taarifa ili sheria ichukue mkondo wake.
“Kama mtaona tofauti yoyote ya jezi tulizozindua na zile zitakazouzwa mitaani ambazo ni feki nyie toeni taarifa ili kuwashughulikia wote wanaotaka kujinufaisha kwa mgongo wa jina la Yanga,’ alisema Msolla ambaye alifichua ile harambee bado inaendelea.
Mwenyekiti huyo kwanza aliwashukuru wanachama wa Yanga kwa kuichangia klabu yao na kuwataka kuendelea kufanya hivyo kwani mahitaji ya timu bado ni mengi.
“Michango yenu imesaidia sana kwenye usajili, lakini bado kuna asilimia 60 ya mahitaji ya fedha na michango mingine kwa ajili ya mishahara ya wachezaji na hata usafiri, posho na malazi katika msimu mpya wa ligi, hivyo niwaombe muendelee kuichangia timu yenu.”
Kuhusu kuchechemea kwa timu Dk Msolla alisema; “Kuna watu wanasema timu mbovu kwa haya Mashindano ya Caf yanayoendelea, ila niwaambie timu iko vizuri ni maboresho tu madogo madogo yanayofanyiwa kazi lakini mtaona uzuri wa timu kwenye Ligi Kuu.”
Katika hatua nyingine alisema uongozi wao umebariki Mikoa ya Kanda ya Kaskazini kuomba kuandaa Wiki ya Mwananchi ili kuichangia klabu yao inayotarajiwa kufanyika wiki ya mechi kati ya Yanga na Alliance mkoani Mwanza.
“Tumefurahishwa sana na mkoa huo kuomba kufanya Wiki ya Mwananchi na tunakaribisha mikoa mingine kuichangia timu yao kwa namna hiyo maana bado mahitaji ni mengi.”
Wiki ya Mwananchi ilifanyika Agosti 4 ikiwa ni miezi kadhaa tangu ilipoasisiwa kupitia Harambee ya Kubwa Kuliko iliyofanyika Juni 15 mwaka huu na kukusanywa kiasi cha Sh920 milioni zikiwamo ahadi na fedha taslimu zilizotumia kukamilisha usajili wa nyota wa kikosi kipya cha msimu huu.
No comments:
Post a Comment