Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile amewaagiza watendaji wa Wilaya ya Kigamboni kuhakikisha Kamati za ulinzi wa Wanawake na watoto zinatekeleza majukumu yake ipasavyo kwa kuisadia jamii ya wanakigamboni kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia .
Dkt. Ndugulile amesema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati wa akizindua Kamati ya ulinzi ya wanawake na Watoto ya Wilaya ya Kigamboni pamoja na Kampeni mpya ya Kitaifa ya kupinga vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto ijulikanayo kama Twende Pamoja inayolenga kushirikisha wanaume na wanawake kwa lengo la kutoa elimu kwa jamii kupitia mbinu anwai.
Aidha Dkt. Ndugulile amesisitiza kuwa Kamati hizo ikisimamiwa vizuri itakuwa nuzo bora katika mapambano dhidi ya vitendo vya kikatili vinavyozidi kushamiri kila siku nchini katika jamii na familia zetu.
Ameongeza kuwa kuwepo kwa elimu bure nchini kwa kiasi kikubwa kumepunguza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake ikiwemo mimba na ndoa za utotoni pamoja na uwepo wa Sheria inayotoa adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela kwa anayebainika kufanya vitendo hivyo.
”Ni matarajio yangu kwamba kampeni hii ya Kupinga Ukatilili wa Kijinsia Kitaifa italeta mabadiliko makubwa kupitia jumbe mbalimbali zilizoandaliwa kupitia muziki, machapisho, nyimbo, shuhuda na Semina zitakazokuwa zinaendelea kutolewa kwenye majukwaa mbalimbali kipindi cha kampeni’’ alisema Dkt. Ndugulile.
Dkt. Ndugulile pia ameagiza kutafutwa kwa wale waonafanya vitendo vya kikatili katika wilaya ya Kigamboni na Tanzania kwa ujumla na vyombo husika kusimamia na kuhakikisha wanawake na watoto wanapata haki zao.
Akizungumzia hali ya ukatili wa kijinsia nchini Dkt. Ndugulile amesema taarifa ya hali ya Uhalifu nchini ya Mwaka 2017 inaonesha kuwa jumla ya watu 41,416 waliofanyiwa ukatili wa kijinsia walitoa taarifa kwenye vituo vya polisi ikilinganishwa na watu 31,996 waliofanya hivyo mwaka 2016.
Dkt. Ndugulile ameyataja baadhi ya matukio ya ukatili yaliyotolewa taarifa kuwa ni ubakaji, vipigo, matusi, ulawiti, kutupa watoto, ukeketaji na kuwapa mimba wanafunzi na kuongeza kuwa kati ya mataukio hayo 41,416 yaliyotolewa taarifa mwaka 2017 matukio 27,703 sawa na asilimia 67 yalifanywa dhidi ya wanawake na watoto.
Dkt. Ndugulile ameongeza kuwa asilimia 40 ya wanawake wa umri kati ya miaka 15-49 wamefanyiwa ukatili wa kimwili au kingono mara moja au zaidi katika kipindi hicho cha maisha wakati wanawake asilimia 20 wenye umri miaka 15-49 wamefanyiwa ukatili wa kimwili katika kipindi cha miezi 12 iliyopita.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Mhe. Sarah Msafiri amesema kuwa Serikali ya Wilaya itahakikisha wanapambana na vitendo vya kikatili na amewaomba wanawake kutoa taarifa ya vitendo hivyo na kuwataka kutofumbia macho vitendo hivyo na kuacha vipite kwa mwavuli wa ndoa.
“Sisi Serikali tunaheshimu ndoa na dini zote ila tunaangalia uhai wa mwananchi hivyo wanawake wenzangu nawaomba ndoa zisiwe sababu ya kuendelea kufanyiwa vitendo vya kikatili na kuachana inawezekana” alisema Mhe. Sarah
Naye mmoja wa wnawake aliyefanyiwa vitendo vya kikatili Bi. Lucy Sanga ameishukuru Serikali ya Wilaya ya Kigamboni kwa kumsaidia kupambana na vitendo vya manyanyaso ambavyo anafanyiwa na mume wake.
“Mume wangu amekuwa akininyanyasa sasa kwa muda mrefu na imefikia hatua ya kuficha vyombo vya kupikia na kunihamisha chumba chetu cha kukaka na kumleta mama yake mzazi kutoka Musoma na yeye analala humo na me nalala kwenye chumba cha watoto” alilalama Bi. Lucy
No comments:
Post a Comment