Baada ya Mfumo wa Kupokea Malalamiko ya Wananchi dhidi ya utendajikazi wa watumishi wa Umma kuonyesha mafanikio makubwa ambapo hadi sasa umekamilika 99% na unatarajiwa kuzinduliwa Rasmi mwishoni mwa mwezi huu, sasa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda amewaita tena Wataalamu wa ICT kufika ofisini kwake kwaajili ya Kuunda Mfumo wa Kusajili ndoa zote zilizofungwa kwa lengo la kuwalinda wanawake dhidi ya Wanaume walaghai wenye mchezo wa kutoa ahadi ya kuoa na mwisho wa siku wanaingia mitini.
RC Makonda amesema mfumo huo utasajili ndoa zote zilizofungwa kidini ikiwemo za Kikristo,Kislamu na zile zilizofungwa Kiserikali pamoja na kuchukuwa taarifa za Idadi ya watoto ndani ya ndoa.
Aidha RC Makonda amesema lengo la jitiada zote hizo ni kumlinda mwanamke dhidi ya Matapeli wa Mapenzi ambao wamekuwa na mchezo wa kuwachezea kinadada kwa kuwaahidi kuwa watawaoa na pindi wanapopata kile wanachokitaka wanaingia mitini jambo linalowaumiza wanawake na kupelekea baadhi yao kutaka kujiua, kupunguza ufanisi wa kazi na pia wengine kujikuta wanawachukia wanaume bila sababu yoyote.
Pamoja na hayo RC Makonda amesema mpango huo pia unalenga kuzilinda ndoa zilizofungwa zisivunjike jambo litakalosaidia ustawi bora wa familia.
Mhe. Makonda amesema Mpango huo haulengi kuwatetea wanawake pekee bali hata wanaume waliowahi kuwagharamikia wanawake kwa kuwasomesha, kuwajengea nyumba, biashara na kuwapatia magari wanayo haki ya kurudishiwa gharama walizotumia.
No comments:
Post a Comment