FAMILIA ya aliyekuwa Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP Limited, Marehemu Dkt. Reginald Mengi imewasilisha pingamizi katika Mahakama Kuu, ikipinga wosia wa Mengi aliouandika kabla ya kifo chake ukiwa na maelekezo ya mgao wa mirathi na mali zake.
Katika pingamizi hilo ambalo limetolewa na mdogo wa marehemu Mengi, Benjamin Mengi baada ya tangazo kutoka kwenye Gazeti la Daily News la Julai 30, 2019, na wosia huo kuwasilishwa mahakamani hapo, Benjamin amedai kwamba, wakati kaka yake, Dkt. Mengi akiandika wosia huo alikuwa amechanganyikiwa.
Kesi kiyo ya mirathi namba 39, ya mwaka 2019 imepangwa kusikilizwa Septemba 16, 2019 na Jaji Josi Myambina. Upande wa pingamizi unaongozwa na Wakili Nikael Tenga huku upande wa usimamizi wa mirathi ukiongozwa na wakili Elisa Msuya.
Aidha, mahakama hiyo imewaamuru waliowasilisha pingamizi hilo kuwasilisha ushahidi mahakamani hapo kabla ya Agosti 28, mwaka huu.
Katika wosia aliouandika Dkt. Mengi Agosti 17, 2017 umewataja wasimamizi wanne wa mirathi ambao ni Benson Benjamin Mengi, William Mushi ambaye ni Msimamizi Mkuu wa Bonite Bottle Ltd na Silvia Mushi ambaye ni Mwanasheria wa Makampuni ya IPP.
Wosia huo umewataja warithi wa mali za Mengi kuwa ni mjane wake Jackline Mengi, watoto wake, Jarden Mengi na Ryan Mengi.
Baadhi ya mali alizoacha mengi ni fedha, ardhi, magari, nyumba na hisa zake zote kwenye makampuni yake yote. Makampuni ya IPP Limited, IT, The Guardian, Info com Ltd na mengine. Nguo za marehemu, saa, cheni ni vingine amewaachia watoto wake Jarden na Ryan,
Pia, imeelezwa kuwa, Mengi ameandika kwamba ameacha kutoa urithi kwa baadhi ya warithi wake kwa makusudi na endapo mtu atapinga mahakamani wosia huo na akashinda, basi apewe Tsh 1000 tu.
No comments:
Post a Comment