Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameagiza kupelekwa timu maalum kuchunguza idara ya Ardhi katika Manispaa ya Shinyanga kutokana na idara hiyo kubainika kupunguza kiasi cha fedha kwa baadhi ya wadaiwa wa kodi ya pango la ardhi katika madeni wanayodaiwa.
Dkt Mabula alitoa maagizo wakati akifunga mkutano wa siku tatu Wataalamu wa sekta ya Ardhi uliomalizika jana jijini Dodoma.
Alisema, sekta ya ardhi katika Manispaa ya Shinyanga imekuwa na mchezo mchafu wa kuwapunguzia wadaiwa sugu wa wa kodi ya pango la ardhi kiasi cha fedha kwa kucheza na mfumo na hivyo kuikosesha serikali mapato kupitia sekta hiyo. ‘’Manispaa ya Shinyanga kuna madudu ya mchezo wa kupunguza madeni, mtu anadaiwa milioni 20 halafu anapunguziwa deni lake hili haliwezi kuvumulika’’ alisema Dkt Mabula
Mbali na mchezo, Naibu Waziri wa Ardhi alisema, Manispaa hiyo imekuwa pia ikiandaa hati nyingi kwa udanganyifu na kusisitiza kuwa timu maalum ya uchunguzi lazima ipelekwe ili kubaini udanganyifu huo kwa kuwa manispaa hiyo imetia aibu na kuondoa uaminifu kwa serikali.
Sambamba na hilo, Dkt Mabula alishangazwa na idara ya ardhi katika Manispaa hiyo kushindwa kufuatilia hati za madai ilizowapelekea wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi na kusubiri Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi wilaya kuwakumbusha jambo alilolieleza kuwa ni kinyume na taratibu za utendaji kazi.
Akigeukia suala la makusanyo ya kodi ya pango la ardhi tangu kuanza kwa operesheni maalum ya kufuatilia wadaiwa sugu wa kodi hiyo, Dkt Mabula alisema zoezi hilo limekuwa na mafanikio makubwa kwa kuwa Wizara imefanikiwa kukusanya bilioni 20 ndani ya mwezi mmoja jambo ambalo halijawahi kutokea.
Kwa mujibu wa Dkt Mabula, Wizara ya Ardhi sasa sasa inaanza utendaji wa kimatokeo badala ya kusubiri hadi mwisho wa mwaka ndiyo ianze ufuatiliaji wa wadaiwa kodi ya pango la ardhi na kubainisha kuwa lengo katika mwaka wa fedha 2019/2020 ni kukusanya bilioni 180.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameziagiza halmashauri za wilaya nchini kuainisha maeneo yote ya wazi kwa lengo la kubaini maeneo yaliyovamia na kutuma taarifa ya matokeo ya zoezi hilo Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ifikapo Oktoba 1, 2019.
Naibu Waziri Mabula alisema, maeneo mengi ya wazi yamevamiwa kwa kuwa baadhi ya watendaji wa sekta ya ardhi wasio waaminifu wameuza ama kutoa vibali vya ujenzi katika maeneo hayo bila kufuata taratibu na hivyo kusababisha kukosekana maeneo ya wazi. ‘’Tuwe na tabia ya kutunza maeneo ya wazi baadhi ya watendaji wameuza maeneo hivyo maeneo yote yapitiwe upya na yale yaliyovamiwa kwa kiasi kidogo taratibu za kuwaondoa zifanyike na Oktoba 1, 2019 taarifa kuhusiana na zoezi hilo ziwe zimefika wizarani .
Pia Dkt Mabula amepiga marufuku ofisi za ardhi katika halmashauri kukodisha vifaa vya upimaji pale ambapo kuna vifaa vya Wizara na kusisitiza kuwa halmashauri hizo zinaweza kuazima vifaa pale tu ambapo kuna idadi kubwa ya wananchi wanaotaka kupimiwa huku vifaa vilivyopo vikiwa havitoshi.
Vile vile, alizitaka halmashauri wakati wa kuchukua makampuni kwa ajili ya kupima maeneo kama vile urasimishaji kuzingatia zile kampuni zenye uwezo na kasi ya kufanya kazi hiyo badala ya kuchukua zile ambazo utendaji unategemea fedha kutoka kwa wapimiwa na kuzionya zile halmashauri ambazo hazijaomba kupima maeneo.
Kwa upande wake Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi aliwataka washiriki wa mkutano huo kuhakikisha wanabadilika kwa kutatua kero za wananchi na kusisitiza kuwa migogoro ya ardhi katika maeneo yao lazima imalizwe haraka badala ya kusubiri viongozi wa kitaifa waende kuitatua .
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Drothy Mwanyika aliwaambia washiriki kuwa ana imani baada ya mkutano kutakuwa na mabadiliko katika sekta hiyo na Wizara ya Ardhi inaandaa mkakati kwa ajili ya kuleta mabadiliko na kitaundwa kikosi kazi vcha kufuatilia.
Mkutano huo wa siku tatu umehusisha Maafisa Ardhi, Wathamini, Maafisa Mipango Miji, Wapima, Wakurugenzi wa Halamashauri pamoja na Makatibu Tawala wa mikoa.
No comments:
Post a Comment