Aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, January Makamba amemshukuru Rais Dk. John Magufuli kwa kumuamini na kumteua kushika wadhifa huo.
Makamba ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli (CCM), uteuzi wake ulitenguliwa jana Jumapili Julai 21 na nafasi yake kuchukuliwa na aliyekuwa Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene.
Kupitia ukurasa wake wa Twitter leo Julai 22, Makamba ameandika ujumbe wa kumshukuru Rais Magufuli saa chache baada ya kuwaapisha Waziri Simbachawene na Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe ambaye amechukua nafasi ya Innocent Bashungwa aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara.
“Neno la mwisho kwenye hili: Namshukuru Rais kwa kuniamini, Makamu wa Rais kwa kunielekeza, PM (Waziri Mkuu) kwa kunisimamia, na Team ya VPO (Ofisi ya Makamu wa Rais), NEMC (Baraza la Taifa la Uhifadhi na Mazingira) na Mawaziri wote kwa ushirikiano.
“Nampongeza Hussein Bashe na Simbachawene kwa kuaminiwa, Nawatakia heri na kuwaahidi ushirikiano wangu wa dhati,” ameandika Makamba.
Aidha huu sio ujumbe wa kwanza Makamba kuandika, aliandika ujumbe mwingine saa chache baada ya taarifa za uteuzi wake kutolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu ambapo pia alitumia ukurasa wake wa Twitter ambapo aliandika “Kwa kweli nimeyapokea mabadiliko yaliyofanywa kwa moyo mweupe kabisa kabisa. Nitasema zaidi siku zijazo.”
No comments:
Post a Comment