Kesi ya uhujumu Uchumi namba 36 ya mwaka 2019, inayomkabili, Shamim Mwasha (41) na Mumewe Abdul Nsembo maarufu kama Abdulkandida (45), leo Julai 22, imeshindwa kuendelea kusikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kwa kile kiilichoelezwa kwamba upelelezi bado haujakamilika.
Kesi hiyo ya usafirishaji wa madawa ya kulevya imeahirishwa hadi Agosti 5, 2019, ambapo bado inasubiriwa ripoti ya Mkemia Mkuu wa Serikali.
Akizungumza mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Kazi Kisutu, Wakili wa upande wa mashtaka, Wankyo Simon amesema kinachosubiriwa kwa sasa ni majibu ya kielelezo kutoka kwa Mkemia na kuomba tarehe nyingine ya kesi hiyo kutajwa.
Mara baada ya maelezo hayo, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Kelvin Mhina aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 8, na washtakiwa wamerudishwa rumande.
Shamim na Mumewe wanashtakiwa kwa kosa la usafirishaji wa madawa ya kulevya aina ya heroin kinyume cha sheria, ambapo wanadaiwa kutenda kosa hilo, Mei 1, 2019 nyumbani kwao maeneo ya Mbezi Beach, ambapo walikutwa na dawa hizo zenye uzito wa gram 232.70.
No comments:
Post a Comment